Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizi majumbani waibuka Mtwara, mkuu wa wilaya aibiwa

53049 WATUMISHI+PIC

Fri, 19 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Polisi mkoani Mtwara inawashikilia watu 23 wakiwamo watumishi wawili wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa tuhuma za wizi wa mali mbalimbali.

Miongoni mwa watu hao wanatuhumiwa kuiba, kompyuta mpakato (4), kompyuta desk top moja na monitor 4, TV (8), deki (4), pikipiki (6), bajaji (1), solar panel (11) betri za gari (3) mitungi ya gesi (17) na redio mbili, kutoka kwenye nyumba za watu mbalimbali, ofisi ya Manispaa ya Mtwara Mikindani na nyumbani kwa mkuu wa wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Aprili 18, 2019 Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Blasius Chatanda amesema watu hao wamekamatwa kufuatia operesheni maalumu inayoendelea ya kuhakikisha wanadhibiti na kutokomeza vitendo vya uhalifu.

Amesema operesheni hiyo inafanyika maeneo ya nchi kavu, baharini na maeneo ya kuingia na kutoka nje ya mkoa na nje ya nchi baada ya kuanza kujitokeza vitendo vya wizi majumbani na ofisini.

“Kufuatia hali hii (operesheni) tunategemea Mtwara itakuwa salama kwa sababu haiwezekani mtu alime korosho baada ya mwaka anunue pikipiki akijua itamsaidia, au mali nyingine yoyote halafu mtu kwa dakika moja au tatu anayetegemea kutajirika kwa haraka ainyakue sio sahihi,” amesema Chatanda.

Hata hivyo, Chatanda amewataka walioibiwa kwenda polisi kutambua mali zao na kuwatahadharisha wenye nia ya kufanya uhalifu mkoani humo.

“Wanaodhani Mtwara ni mahali sahihi pakuja kufanya   uhalifu watafute shughuli nyingine ya kufanya kwa sababu sheria haitawacha salama na tutawashughulikia kwa nguvu zote kwa mujibu wa sheria, tutaubomoa na kuufuta mtandao wote,” amesema Chatanda.

 

Wakati huohuo, Kamanda Chatanda amesema wamekamata zana za uvuvi haramu na sumu inayotumika kuua samaki baharini.

“Hii ni sumu ambayo ikishatumika au kuwekwa kwenye maji samaki aidha wanakufa na wavuvi kuwapata kirahisi kama ambavyo tumekuwa tukisikia samaki waliovuliwa kwa sumu wana madhara pia kuna madhara kwenye mazalia, niwaombe na wananchi waendelee kutupa taarifa,” amesema Chatanda.

Mkazi wa Mtwara, Faruku Adam amepongeza operesheni hiyo na kuomba wananchi kuwafichua wahalifu na kutoa taarifa wanapowaona watu wasiowafahamu katika maeneo yao.

“Ni operesheni nzuri wananchi tutaendelea kushirikiana na polisi tunapoona vitendo vya uhalifu kwa sababu kama wezi wanaiba mpaka nyumbani kwa mkuu wa wilaya itakuaje kwa sisi raia wa kawaida?” amehoji Adam.



Chanzo: mwananchi.co.tz