Watendaji wa Kata, Kijiji pamoja na vibarua tisa waliokua wakifanya shughuli ya kupokea misaada ya waliokumbwa na mafuriko wilayani Rufiji wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, kwa tuhuma za wizi wa vyakula vya misaada inayotolewa na serikali na Wahisani mbalimbali kwa watu waliokumbwa na mafuriko Wilayani humo.
Akielezea tukio hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya maafa ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Eward Gowele amesema watuhumiwa hao wanashikiliwa TAKUKURU kwa mahojiano huku akiwaonya wanaopewa dhamana ya kusimamia misaada hiyo kutojihusisha na wizi wa misaada hiyo.
Alisema, wapo Mtendaji wa Kata na Kijiji ambao walikiuka miongozo kwa kutoa chakula au kwa kujigawia chakula nje ya utaratibu huku wakijua wazi wao sio waathirika wa mafuriko na tayari wamechukuliwa hatua ambapo TAKUKURU wanaendelea na uchunguzi dhidi yao.
“Pia wapo vijana ambao tunawatumia kwa kazi za vibarua wa kushusha mizigo nao walifanya hivyo TAKUKURU waliwakamata vijana hao tisa ambapo wanaendelea kushughulika nao kwa mujibu wa sheria,” alisema Meja Gowele.