Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara kudhibiti ndege Selengwa

24c5f9bb287b7b2aa9016b905505a123 Wizara kudhibiti ndege Selengwa

Wed, 7 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Kilimo imepanga kupeleka wataalamu na vitendea kazi mkoani Singida Mei hadi Julai mwaka huu kwa ajili ya kudhibiti ndege aina ya Selengwa.

Sambamba na hilo, serikali inafanya mazungumzo na mashirika ya kimataifa kama Benki ya Dunia kupata ndege za kutosha kunyunyizia dawa kwa ndege na wadudu waharibifu badala ya kutegemea ndege za mashirika ya nje.

Katika kuboresha hilo, katika bajeti inayotarajiwa kuwasilishwa hivi karibuni, Wizara ya Kilimo itaongeza bajeti kukiboresha Kituo cha Kilimo Anga.

Mei mwaka jana, wizara hiyo ilipeleka wataalamu Mkoa wa Singida kwa ajili ya kutambua maeneo yenye mazalia ya ndege hao na kubaini kuwepo katika vijiji 12.

Vijiji hivyo ni Pohama, Ngimu, Muhanga, Mguli, Mkola na Shahana katika wilaya ya Singida; Ushora, Urughu na Mlandala vilivyopo wilaya ya Iramba na Ighombe, Mghungira na Iyumbu vilivyopo wilaya ya Ikungi.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema mbinu ya kuwadhibiti ndege hao ni tofauti na ile ya kudhibiti ndege aina ya Kweleakwelea wanaodhibitiwa kwa kutumia kiuatilifu aina ya Fenthion kinachonyunyizwa kwa kutumia ndege.

“Kutokana na uwezo mkubwa wa ndege aina ya Selengwa kusikia sauti ya ndege inayonyunyizia kiuatilifu na tabia yake ya kujificha, udhibiti kwa kutumia mitego umeonesha ufanisi zaidi. Hivyo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, halmashauri pamoja na wakulima itaendelea kuwadhibiti ndege hao kwenye maeneo watakakobainika wakishambulia mazao,” alisema Bashe.

Alikuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM) aliyehoji “Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima wa Jimbo la Singida Magharibi wanaoteswa na ndege aina ya Selengwa kula mazao yao na kuwarudisha nyuma kiuchumi?”

Ndege Selengwa ni moja ya aina ya kasuku wadogo waliopo nchini. Ndege hao wapo kwenye uhifadhi wa dunia kisheria kama wanyama walio hatarini kutoweka toka mwaka 1985.

Aidha, ndege hao sio wahamaji na hula mazao ya alizeti, mahindi, mtama na baadhi ya matunda. Ndege mmoja anaweza kula kati ya gramu 45 hadi 60 kwa siku hivyo kundi lenye ndege milioni moja linaweza kula kati ya tani 45 hadi 60 ya nafaka kwa siku moja.

Bashe alisema, “kwa ulaji huu idadi ya ndege Selengwa isipodhibitiwa inaweza kuleta madhara ya kiuchumi kwa wakulima.”

Kuanzia mwaka 2004 idadi ya ndege hao imekuwa ikiongezeka na kuonekana katika maeneo ya Manyoni, Bahi, Singida, Iramba, Meatu na katika hifadhi ya Serengeti.

Aidha, kukua kwa shughuli za kilimo hadi kwenye makazi ya asili ya ndege hawa pia kumechangia mwingiliano wa ndege hawa na binadamu.

Bashe alisema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ilituma wataalamu kufanya tathmini na kubaini ndege hao waliharibu asilimia 30 ya mazao katika kipindi cha mwaka 2004.

Aidha, Wizara ya Maliasili kwa kuzingatia taratibu za uhifadhi wa ndege hao ilitoa kibali cha kuwadhibiti ambapo mwaka 2006 Wizara ya Kilimo ilifanya udhibiti maalumu kwa kutumia mitego.

Chanzo: www.habarileo.co.tz