Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wilaya ya Gairo na maliasili adimu isiyopatikana kwingine

09d246381589a9ecd29692269ef62f4c.png Wanyama wanaopatikana Gairo

Fri, 17 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WILAYA ya Gairo ilianzishwa Machi 02, 2012 kutokana na kugawanywa kwa Wilaya ya Kilosa, na baadaye utekelezaji wa shughuli zake ulianza rasmi Julai 2013.

Gairo inapatikana Kaskazini Magharibi mwa Mkoa wa Morogoro na inapitiwa na barabara kuu ya Morogoro- Dodoma. Wilaya hii ni miongoni mwa maeneo machache duniani yenye vivutio vingi adimu vya utalii ikiwemo; Safu za milima ya Rubeho na Ukaguru ambayo ni sehemu ya milima inayounda Safu za Milima ya Tao la Mashariki (Earstern Arc Mountain).

Pia yapo magofu ya kale; alama ya unyayo wa mwanadamu wa kale katika Kijiji cha Nguyami; vyura adimu duniani waitwao vyura Filimbi; ndege adimu duniani aina ya Rubeho warbler na Moreaus sunbirds, ambao wanapatikana wilayani Gairo pekee (Endemic species).

Kuna maporomoko ya maji ya Ukaguru pamoja na mimea mbalimbali katika hifadhi za misitu asilia ya Mamiwa Kaskazini, Ikwamba, Italagwe na Hifadhi ya Msitu wa Mipingo (Leshata Vipigo Forest).

Kwa nini mimea na wanyama wa misitu ya milima ya Rubeho na Ukaguru ni muhimu? Kwanza hii sehemu ya misitu ya Milima ya Tao la Mashariki. Pili, misitu ya milima ya Rubeho ni muhimu sana kwa sababu inalinda vyanzo vya maji na udongo na hutoa mimea itumikayo kama dawa.

Ni muhimu zaidi kwa sababu inategemewa na aina nyingi za mimea na wanyama. Baadhi ya hii mimea na wanyama haipatikani mahali pengine duniani. Kama hiyo haitoshi, misitu hii ni muhimu sana kwa sababu inahifadhi mimea na wanyama aina mbalimbali ambao, kwa mujibu ya machapisho mbalimbali, hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani.

Kama misitu hii itafyekwa basi viumbe hawa watatoweka. Misitu hii pia inahifadhi hewa ukaa; inalinda vyanzo vya maji; na pia inatoa dawa za asili za miti shamba pamoja na mazao mengine ya misitu kwa jamii.

Tunajuaje kuna wanyama na mimea kwenye misitu hii? Kupitia mradi wa MKUHUMI (Mkakati wa Kupunguza Ukataji Miti ovyo na Uharibifu wa Misitu) timu ya wataalamu kutoka Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), wakishirikiana na wanajamii, watalaamu wa kienyeji wa miti shamba na wanasayansi, wamekuwa wakijifunza na kujua zaidi kuhusu mimea na wanyama wanaopatikana katika misitu hii. Kwa kutumia mbinu mbalimbali za kutafiti za kisayansi, wataalamu hao walibaini aina mbalimbali za wanyama na mimea.

Timu hii pia imepiga picha za wanyama na mimea na imechukua baadhi ya sampuli za mimea kwa ajili ya utafiti zaidi. Utalii unaofanyika katika eneo hilo ni pamoja na utalii wa kupanda milima, utalii wa picha, utalii wa ndege na wanyama wadogowadogo kama vile vyura filimbi, kwale na kanga wa rubeho, kima, tumbili na nyani, utalii wa utafiti, utalii wa utamaduni (ngoma, vyakula vya asili, michezo, matambiko, ibada na maziko/mazishi).

Kwa mujibu wa machapisho, kuna zaidi ya aina 132 za ndege, aina 40 za mamalia (wanyama wanyonyeshao), aina 14 za wanyama jamii ya nyoka na mijusi na aina 14 za wanyama jamii ya vyura ambao wanaishi katika misitu hii ya milima ya Rubeho na Ukaguru. Aina nyingi za wanyama hawa wanaishi tu msituni na watakufa endapo misitu hii ikiharibiwa.

Baadhi ya misitu muhimu katika milima ya Rubeho ni pamoja na Mafwemela, Ipondelo, Mang’alisa, Ukwiva na Ilole. Kwa sasa misitu hii ipo katika hatari kubwa ya kuathiriwa na ukataji wa miti kiholela, uchomaji moto na ufyekaji kwa ajili ya kilimo na shughuli zingine za kibinadamu.

Wanyama wanaopatikana kwenye Misitu ya Rubeho na Ukaguru ni pamoja na Nike’s squeaker; hawa ni aina ya vyura ambao wanaishi kwenye misitu ya Milima ya Rubeho tu. Ni vyura adimu sana na wanahitaji misitu ili waweze kuishi.

Kuna vinyonga wenye pembe tatu (Werner’s chameleon) ambao wanapatikana kwenye misitu ya Milima ya Rubeho na kwenye baadhi ya misitu ya Milima ya Tao la Mashariki.

Pia kuna vinyonga vya aina tofauti zisizopungua nne katika misitu ya milima hii ya Rubeho na Ukaguru. Komba wa mlimani pia wanapatikana kwenye misitu iliyoko kwenye milima ya Rubeho.

Hawa komba ni aina adimu na wapo kwenye tishio la kutoweka kutokana na uharibifu wa misitu hii. Komba hula wanyama wadogo na gundi itokanayo na miti. Hufanya shughuli zake usiku na kulala mchana.

Wanyama wengine adimu ndani ya misitu hii ni Minde, hawa ni funo wa msituni ambao pia wako kwenye tishio kubwa kutokana na uwindaji. Minde wanapatikana kwenye misitu michache ikiwemo ya milima ya Rubeho.

Kwenye baadhi ya misitu ya Tanzania kama Tanga, ambapo walikuwa wanapatikana kwa wingi sasa wametoweka kabisa kutokana na uwindaji na uharibifu wa msitu. Nyoka wa msitu wa Uluguru wanapatikana katika Milima ya Tao la Mashariki pekee.

Nyoka huyu alipatikana miaka ya karibuni katika msitu wa Ilole. Kwa upande wa ndege wapo kwale wa Rubeho ambao ni aina ya ndege adimu sana wanaopatikana kwenye misitu ya Milima ya Rubeho pekee na hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani. Kutokana na machapisho kadhaa imebainika kuwa aina hii ya ndege ni wachache sana duniani hivyo ni muhimu watu wasiwawinde na kuwaua.

Pia kuna aina nyingine ya ndege wasiopungua 78 katika misitu ya milima ya Rubeho. Wanyama wengine walio katika hatari ya kutoweka ambao wanaishi kwenye misitu michache ya Tanzania ikiwemo misitu ya Milima ya Rubeho ni Kanu ya Lowe (Lowe’s servaline genet). Mnyama huyu yuko kwenye tishio la kutoweka kutokana na ufyekaji wa misitu na uwindaji.

Ukimuondoa popo, kuna aina tofauti ya wanyama wanyonyeshao wasiopungua 31 kwenye misitu hii. Imegundulika pia kuna aina mpya ya chura ndani ya misitu ya Milima ya Rubeho.

Aina hii adimu ya chura haijawahi kutambuliwa na wanasayansi wowote mpaka timu ya wataalamu kutoka TFCG na MJUMITA walipotembelea eneo hilo. Chura huyu amegundulika kutoka kwenye eneo la msitu mdogo ujulikanao kama Mikuvi ambao ni sehemu ya msitu wa hifadhi wa Kijiji cha Kisongwe. Ili aina hii ya chura iweze kuishi, ni muhimu kuhakikisha msitu huu unahifadhiwa.

0685 666964 au bjhiluka@ yahoo.com

Chanzo: habarileo.co.tz