Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenye watoto Albino wapewa somo kuelekea uchaguzi mkuu Tanzania

Wenye watoto Albino wapewa somo kuelekea uchaguzi mkuu Tanzania

Mon, 9 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Under The Same Sun limewataka wanawake wenye watoto wenye Albino  kuwaongezea ulinzi watoto wao  hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

Pia, limewataka wanawake hao kutosita kuwashtaki wanaume wasiotoa matunzo ya watoto wao kwa sababu ya Ualbino hata kama wanao uwezo wa kufanya hivyo.

Mwanasheria wa shirika hilo, William Maduhu amesema hayo leo Jumamosi Machi 7,2020 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanawake wenye watoto albino ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kesho Machi 8, 2020.

“Jukumu la kwanza la ulinzi ni familia, wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi wazazi wajue watoto wao wanapoenda kucheza wapo na akina nani na wanarudi saa ngapi,” amesema Maduhu

“Mkiona kuna viashiria vyovyote vya  kuhatarisha usalama wa watoto wao watoe taarifa kwenye ofisi za Serikali za mtaa au polisi, nyie mnatakiwa kuwa walinzi namba moja.”

Amesema walau matukio ya ukatili dhidi ya albino yamepungua japo suala la unyanyapaa bado lipo.

Pia Soma

Advertisement

“Kuanzia Jumatatu wazazi wenza walio telekeza watoto muwapeleke kwenye vituo vua ustawi wa jamii, sheria inawalinda watoto,” amesema Maduhu.

Awali, mshauri wa masuala ya malezi kwa watoto, Grace Wabanhu aliwataka wanawake hao kuwa jasiri kwa kuhakikisha wanawalinda watoto wao na kusimamia haki zao zote za msingi.

“Kina mama mnapaswa kutambua mahitaji ya msingi ya watoto wenye ualbino na niwasihi mpambane kufa na kupona msiwaache watoto wenu, msikubali kukata tamaa hata kama mmeumizwa na wazazi wenzenu,” amesema Grace.

Amesema waitumie siku ya maadhimisho ya wanawake kama njia ya kuwasamehe wazazi wenzao waliowakataa na kutelekeza watoto ili wasipandikize chuki kwa watoto wao.

“Msiwajaze chuki watoto kuwa baba zao waliwakataa, waleeni tu na wakikua waunganisheni na baba zao, mimi na ndugu zangu tulikataliwa na baba lakini mama alitusimamia tukatimiza ndoto zetu bila kupandikizwa chuki, tulimtunza baba mpaka anafariki,” anasema Grace.

Kwa upande wao baadhi ya wanawake hao wamesema changamoto kubwa wanayopambana nayo kwenye malezi ni unyanyapaa.

Chanzo: mwananchi.co.tz