Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenye ulemavu wahakikishiwa neema

3e263326afcf306ca86efdd486c43953 Wenye ulemavu wahakikishiwa neema

Fri, 4 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAKAMU wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdallah amesema watu wenye ulemavu wanaweza kufanikiwa kimaisha kama watu wengine kwa kuzitumia fursa zinazotolewa na serikali na mashirika ya umma.

Alisema Serikali ya Mapinduzi inafahamu ukubwa wa tatizo la watu wenye ulemavu na ndiyo maana imejipanga kulipatia ufumbuzi kwa njia mbalimbali ikiwemo kuzitambua haki na fursa kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu katika ukumbi wa Shehe Idriss Abdull Wakil mjini hapa, alisema suala la elimu kwa watu wenye ulemavu limepewa kipaumbele katika kipindi cha serikali ya awamu ya nane, ikiwemo kuboresha elimu ya mjumuisho.

Alisema serikali inakusudia kuipitia upya sera ya watu wenye ulemavu ili kujua mahitaji yao kamili.

Aidha alisema serikali imejipanga kutekeleza mikataba ya kimataifa kwa watu wenye ulemavu ikiwemo kuhakikisha walemavu wenye sifa wanaajiriwa serikalini pamoja na sekta binafsi.

''Suala la ubaguzi katika ajira tunataka kulipatia ufumbuzi wake wa mwisho....mlemavu yeyote mwenye sifa anaweza kuajiriwa serikalini au katika sekta binafsi,'' alisema.

Awali, akiwasilisha risala ya Shirikisho la Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA), Ali Omar alisema kundi la watu wenye ulemavu limefarijika kwa kiasi kikubwa kutokana na kauli ya Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi kuyashirikisha makundi yote katika ujenzi wa taifa.

Alitaka walemavu kushirikishwa kikamilifu katika fursa zitakazopatikana katika mikakati ya uchumi wa buluu ambayo ndiyo malengo ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza ajira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu wa Baraza la Wawakilishi, Dk Khalid Salum Mohamed alisema wizara inakusudia kuitisha mkutano utakaowashirikisha wadau kwa ajili ya kuipitia sera ya watu wenye ulemavu.

''Kwa vile suala la watu wenye ulemavu ni mtambuka kutokana na kugusa sekta mbalimbali tunakusudia kuitisha mkutano wa wadau

kuijadili na kuipitia sera ya watu wenye ulemavu,'' alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu, Abeda Rashid Abdalla aliipongeza rasimu ya watu wenye ulemavu ya Jamhuri ya Muungano kwa kulitambua rasmi kundi la watu wenye ulemavu pamoja na mahitaji yao kwa ujumla.

''Tumepata moyo na nguvu kupitia rasimu ya watu wenye ulemavu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeyatambua makundi yote ya watu wenye ulemavu pamoja na haki zao kwa ujumla,'' alisema.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kwamba wapo watu wenye ulemavu wapatao bilioni moja sawa na asilimia 15 ya watu wote duniani.

Aidha, kwa upande wa Zanzibar inaonesha watu 8,265 wana ulemavu wa aina mbalimbali huku wanaume ni 4,375 wakati wanawake ni 3,890.

Ujumbe wa kimataifa kwa siku ya watu wenye ulemavu duniqni ni ''Uchumi wa Bluu jumuishi" utatoa fursa kubwa za ajira kwa watu wenye ulemavu.

Chanzo: habarileo.co.tz