Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenye ulemavu kupatiwa miguu bandia

Tue, 22 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zaidi ya watu 120 wenye ulemavu kutoka mikoa mbalimbali nchini watakabidhiwa viungo bandia ili warejee katika hali ya kawaida itakayowasaidia kufanya kazi na kujiingizia kipato.

Walemavu wengi ni wale waliopoteza miguu kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ajali za barabarani na magonjwa.

Bei ya mguu bandia mmoja katika hospitali za rufaa hapa nchini huanzia kati ya Sh1 milioni hadi Sh3 milioni.

Mwenyekiti wa Kamal Group, Gagan Gupta akizungumza leo Jumapili Januari 20, 2019 jijini Dar es Salaam amesema kampuni hiyo inatoa zawadi ya mwaka mpya kwa watu wenye ulemavu ili waweze kufanya kazi za kujipatia riziki na kurejesha furaha yao.

Gupta amesema msaada huo unatolewa kupitia mfuko wake wa Uwezeshaji wa Wananchi (Peoples’ Empowerment Foundation - PEF), Kamal Group kwa kushirikiana na Klabu ya Rotari ya Bahari Dar es Salaam imetoa miguu bandia yenye thamani ya mamilioni ya fedha kwa watu 120.

"Hii ni mara ya nne kwa kampuni ya Kamal kutoa zawadi kwa walemavu na mpaka sasa tumewafikia 370 na waliopata wanaendelea na kazi zao kama kawaida,"  amesema.

Baadhi ya watu wenye ulemavu wamesema zawadi watakayopata inazidi thamani ya pesa kwa sababu baadhi yao walikata tamaa kimaisha kwa kukosa viungo.

"Nasubiri kwa hamu kupata mguu naamini nitaweza kumaliza masomo yangu ya sekondari kwa amani,"  amesema Omary Iddy mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Highland ya mkoani Iringa.

Naye Mbunge wa viti maalum (CCM), Ritha Kabati aliyesafirisha walemavu 25 kutoka katika mkoa wake wa Iringa amesema viungo wanavyopatiwa walemavu hao vitawafanya wengi watimize ndoto zao kimaisha.

"Viungo hivi vitapunguza utegemezi kwa sababu hawa watakaopewa wataweza kufanya kazi na kuinuka upya, kampuni hii imefanya kazi nzuri natamani kuona nyingine zinaiga mfano katika kutatua matatizo ya jamii," amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz