Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenye nyumba za nyasi matatani

1ebfd597a059783ce49f0b32d826899e Wenye nyumba za nyasi matatani

Sun, 3 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ametoa muda wa miaka mitatu kuanzia sasa kwa wakazi wenye nyumba za nyasi, kujenga nyumba zenye hadhi.

Alisema hayo katika ibada ya Krismasi, iliyofanyika Kanisa la Bibilia Tanzania na kuadhimishwa kitaifa mkoani hapa.

Byakanwa alisema wakazi hao wenye nyumba za nyasi, hawastahili kuishi kwenye mkoa wenye utajiri mkubwa wa kilimo na biashara za korosho.

"Baada ya miaka mitatu kuanzia sasa kama unaishi kwenye nyumba ya nyasi na tope utapaswa kutupisha Mtwara, utakuwa sio stahili yetu," alisema.

Aliwataka wananchi wa mkoa huo, kuanza kulima mazao mbalimbali ikiwemo korosho, ufuta na karanga ili waweze kupata fedha za kuboresha makazi yao.

Akiwa katika ziara ya kampeni ya kuhamasisha wananchi kulima kilimo bora cha korosho wilaya mbalimbali, mkuu huyo wa mkoa alisisitiza wananchi kujenga makazi bora na kuachana na nyumba za nyasi.

Alitaka kila mmoja kuwa na shamba ambalo analima mazao, ikiwemo korosho ifikapo Februari mwakani.

Alisema kwa wakazi watakaoshindwa kujishughulisha na kilimo cha mazao, ifikapo Februari wataanza kukamatwa na kutozwa faini na kuazimika kutafuta shamba na kujishughulisha na kilimo kwa manufaa.

Byakanwa alisema kama wakulima watalima, watajipatia kipato cha kuboresha maisha yao na kukuza uchumi wa nchi. Alisisitiza kuwa kuanzia sasa, kila mtu anapaswa kuwa na shamba

Katika ziara hiyo ya baadhi ya wilaya, mkuu wa mkoa aliiambatana na watafiti wa zao la korosho kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) Kituo cha Naliendele, ambao wanafundisha kilimo bora cha korosho ili wakulima wapate mazao mengi kwa kuwa idadi ya mikorosho iliyopo haiendani na mavuno yanayopatikana. Wananchi walieleza kuwa elimu waliyopata itaongeza mapato.

Byakanwa alisema kuwa tathimini waliyofanya kwenye mkoa huo, wamebaini uzalishaji wa mazao umeshuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutelekezwa kwa mashamba na kuwa mapori, kutozingatiwa kwa kanuni za kilimo, sababu za kiikolojia na kutolimwa kwa mazao ya chakula.

Alisema takribani asilimia 70 ya chakula kinacholiwa mkoani Mtwara, kinategemea mazao yanayoingizwa kutoka mikoa mingine, huku asilimia 30 ndicho chakula kinacholimwa ndani ya mkoa na kusababisha gharama za maisha kuwa juu.

Kwa upande wa uzalishaji wa zao kuu la biashara la korosho, alisema katika miaka mitatu mfululizo zao hilo limeshuka kutoka tanii 180,000 kwa mwaka hadi kufikia tani 120,000.

Akizungumzia malengo ya mkoa, Byakanwa alisema wamepanga kuhamasisha wakulima kuondokana na kilimo cha mazoea na kuongeza uzalishaji.

Aidha, mkoa umeanzisha kampeni ya kuondoa mapori na kila wilaya inapaswa kuhakikisha vijana wanashiriki kwenye kilimo ili kuongeza uzalishaji. Kila kaya itapaswa kuwa na eka moja ya kilimo kila mwaka.

Kaimu Mkurugenzi wa Tari Naliendele, Fortunatus Kapinga aliwataka wakazi wa Mtwara kuacha kulima kilimo cha mazoea na kufuatilia mbinu bora za kilimo.

Chanzo: habarileo.co.tz