Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Ummy aagiza uchunguzi Tsh.milioni 50 ujenzi zahanati Hai

Ummy Pic Data Ummy Mwalimu, Waziri TAMISEMI

Thu, 18 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu ameagiza kuundwa kwa kamati ndogo ya uchunguzi wa matumizi ya Sh50 milioni zilizotolewa na Serikali Kuu katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Zahanati ya Chemka baada ya kuibuka utata wa fedha hizo.

Agizo la Ummy linatokana na malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Chemka ambao walidai kuwapo kwa nguvu zao walizochangia na wakati huo huo Halmashauri ya Hai ikidai ndio iliyotoa fedha hizo.

Wananchi wa kijiji hicho walimweleza Waziri Ummy kuwa wamechangia nguvu kazi katika ujenzi huo hadi hatua ya kupaua huku uongozi wa Halmashauri ukidai kutumia Sh50 milioni katika ujenzi wa zahanati hiyo.

Waziri Ummy ametoa agizo hilo wilayani Hai wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo zahanati pamoja na shule mkoani Kilimanjaro.

"Milioni 50 tunaweza kuiona ni ndogo lakini ni kubwa sana, huu mradi wa zahanati ya chemka tumeona namna wananchi wamejenga na sisi hatuwezi kuwaacha wananchi bila kuwaunga mkono, sasa kama tunakuja hapa tunakuta hapajakaa vizuri maana yake kuna shida"

"Namwagiza mkuu wa wilaya ya Hai aunde kamati ndogo ije kukagua matumizi ya Sh50 milioni ili tupate ukweli nani ameezeka hili jengo, Serikali au ni wananchi," ameagiza Waziri Ummy na kuongeza

"Maana yake kama wananchi wameshaezeka Sh20 milioni zingeweza kukamilisha hili jengo, milioni nyingine 20 ingetosha kujenga nyumba ya mtumishi, mimi sijaridhika matumizi ya Sh50 milioni iliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo hili,"

Waziri Ummy amemtaka Mkuu wa wilaya hiyo kumpa taarifa baada ya kamati hiyo kufanya kazi yake ili kama kuna mtumishi yoyote amehusika aweze kuchukuliwa hatua.

"Mkuu wa wilaya niletee taarifa nitafanya maamuzi kama kuna yeyote amehusika hata kama ameondoka hapa Hai, mimi nimesema chini ya uongozi wangu huwezi haribu kwenye Halmshauri hii alafu ukapelekwa Halamshauri nyingine ntakupeleka Takukuru hapa na tutamalizana hapo hapo," amesema Waziri Ummy

Akitoa taarifa ya ujenzi wa zahanati hiyo, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Irene Haule amesema mradi huo ulianza tangu mwaka 2016 ambapo unatarajiwa kukamilika Novemba 30 mwaka huu.

Chanzo: mwananchidigital