Kibondo. Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa ameagiza kusimamishwa kwa shughuli za soko la pamoja baina ya Watanzania na wakimbizi wa kambi ya Nduta wilayani Kibondo kutokana na sababu za kiusalama katika wilaya hiyo na mkoa wa Kigoma kwa ujumla.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumanne Februari 19, 2019 wakati akizungumza na watumishi wa Serikali wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.
Amesema sababu ya kufungwa kwa soko hilo au kulihamishia ndani ya kambi hiyo ni kuzuia wakimbizi wasiweze kutoka nje kwa ajili ya usalama kwani wamekuwa wakitoka na kwenda kufanya shughuli zisizo rasmi.
"Kila mmoja anawajibu wa kulinda mipaka ya wilaya yetu na mkoa kwa ujumla na si kutegemea jeshi la polisi peke yake, lengo ni kuzuia watu kuingia katika mipaka yetu kinyume cha sheria," amesema Waziri Mkuu.
Aidha amekemea kitendo cha wananchi kuvaa sare za kijeshi za nchi yoyote kama siyo mwanajeshi na kuonya atakayefanya hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.