Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mkuu ataka bandari ya Mtwara itumike kushusha mafuta

Bandari Mtwara Mafuta Waziri Mkuu ataka bandari ya Mtwara itumike kushusha mafuta

Sat, 8 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwelekeza Waziri wa Nishati kukaa na wawekezaji wa mafuta bandarini ili kuona namna ya kuwasaidia ili wapate faida kwa kuitumia bandari ya Mtwara.

Majaliwa ameyasema hayo katika ziara aliyoifanya katika bandari ya Mtwara pamoja na Bohari ya mafuta kufuatia malalamiko aliyoyapata kutoka kwa wawekezaji hao jana kuwa kwenye vituo vya mafuta wananunua mafuta Dar es Salaam badala ya Mtwara.

"Waziri mwenye dhamana akae na hao wawekezaji aone namna nzuri ya kuwezesha uwekezaji wao uwe na faida, aone namna ya kuwasaidia wafanye biashara," amesema Majaliwa.

Aidha aliwaelekeza wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma kuwa hakuna haja ya kwenda kununua mafuta Dar es Salaam badala yake wanunulie Mtwara.

"Inawezekana hawajui kwamba kuna mafuta hapa bandari ya Mtwara au makusudi au kampeni chafu," amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Bohari ya Mafuta GM and Company Ltd, Paul Masawe amesema wamekuwa na wakati mgumu wa bei kwani kitendo cha meli kushusha mzigo mkubwa katika Bandari ya Dar es salaam na kuleta mzigo mdogo Mtwara imesababisha bei ya mafuta kupanda.

“Changamoto kubwa ni tofauti ya bei, kwani dizeli tofauti ni Sh400 na kwa uchache wa mafuta yanayoingia Mtwara mara moja kwa mwezi, unasababisha bei kuwa kubwa,” amesema.

Naye Meneja wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mtwara, Mhandisi Said Mkwawa amesema kuwa shirika hilo kwa sasa limesogeza huduma ya upimaji wa mafuta mkoani humo ambapo huchukua masaa manne kwa mafuta ya diseli.

“Tunayo maabara hapa hapa Mtwara tukipokea mafuta tunapima na kutoa majibu Serikali ilishatuelekeza tangia mwaka jana tulianza kupima mafuta hapa Mtwara ingawa Dar es salaam yanapimwa lakini na sisi tunajiridhisha kwakuwa yanakuwa yametembea,” amesema mhandisi Mkwawa.

Chanzo: Mwananchi