Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mkuu acharuka wanafunzi kukatisha masomo kwa kupata mimba

29367 Waziri+pic TanzaniaWeb

Thu, 29 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amechukizwa na vitendo vya wasichana kukatisha masomo yao kwa kupata ujauzito wilayani Nyang’hwale mkoani Geita.

“Tukikukuta umesimama na binti katika kona isiyoeleweka tutakukamata. Ole wenu mtakaobainika kuwapa ujauzito wanafunzi adhabu yake ni miaka 30 jela,” alisema Majaliwa. 2018.

Alitoa kauli hiyo baada ya kupata taarifa kuwa wanafunzi 72 wamepata ujauzito wilayani humo kuanzia mwaka 2016 hadi 2018.

Kufuatia hali hiyo alimuagiza mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale, Hamim Gwiyama kufanya operesheni katika kila kijiji kubaini waliowapa wanafunzi ujauzito na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Sabasaba kijiji cha Kalumwa.

“Jambo jingine litakalowawezesha kukabiliana na tatizo la ujauzito kwa wanafunzi wa kike ni kuanzisha miradi ya ujenzi wa mabweni ili waweze kusoma bila ya kupata vishawishi vinavyosababisha kupata ujauzito,” alisema.

Alisema Serikali haiwezi kuacha jambo hilo liendelee na kuwataka wananchi kushirikiana kuwalinda wanafunzi na kuonya Serikali itawachukulia hatua watendaji wote ambao katika maeneo yao wanafunzi watabainika kuwa na ujauzito.

Pia alitoa onyo kwa wazazi na walezi watakaowaozesha wasichana ambao bado ni wanafunzi na watakaowasindikiza watoto wao wa kiume kwenda kuoa.

Naibu Waziri Tamisemi (Elimu), Mwita Waitara alimueleza Majaliwa kuwa Novemba 30 mwaka huu alirejea wilayani humo kwa ajili ya kuwashughulikia wanaokatisha masomo wanafunzi na  kwamba ametoa namba ya simu ili wananchi waanze kumpa taarifa za wahusika.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo.

Alisema vijiji hivyo vitaunganishiwa umeme katika awamu ya tatu ya Mradi wa Umeme Vijijini (Rea).

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz