Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mgalu azindua mradi wa umeme wa jua Lindi

Mgalu Ed.webp Waziri Mgalu azindua mradi wa umeme wa jua Lindi

Mon, 18 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amezindua mradi wa umeme jua unaoendelea kutekelezwa katika vijiji vya Kata ya Nanjirinji, wilayani Kilwa, mkoani wa Lindi.

Akizungumza na viongozi wa eneo hilo akiwemo Mkuu wa Wilaya, Diwani na viongozi wa vijiji husika, Naibu Waziri ameseleza kuwa mradi huo unalenga kuwapatia huduma ya umeme wananchi hao wakati serikali ikijiandaa kupeleka umeme wa uhakika kupitia mradi wa umeme vijijini (REA).

“Tunashukuru Bunge kwa kupitisha bajeti ya Wizara yetu kwa mwaka wa fedha 2020/21 ambayo ni pamoja na mambo mengine, imejikita katika upelekaji umeme vijijini. Nafurahi kuwajulisha kuwa vijiji vya Nanjirinji ni miongoni mwa vijiji vitakavyopelekewa umeme ndani ya kipindi husika,” amesema Mgalu.

Naibu Waziri ameeleza kuwa mradi huo ni mpango mkakati uliowekwa na serikali kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyo mbali na miundombinu ya umeme mkubwa, vikiwemo visiwa, wanafikishiwa huduma ya umeme ili waweze kunufaika sawa na wananchi wa maeneo mengine.

Hata hivyo, Mgalu amewataka Mawakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao ndio wafadhili wa miradi ya aina hiyo kote nchini, kujenga utaratibu wa kutembelea miradi hiyo ili kujiridhisha kama fedha zilizotolewa na wadau wa maendeleo katika kutekeleza miradi hiyo zinatumika ipasavyo.

Pia amewataka Mawakala huo kuanzisha kitengo cha tathmini na ufuatiliaji, ambacho kitashughulikia masuala hayo katika miradi yote ya umeme jadidifu.

Wakati huohuo Naibu Waziri ametumia fursa hiyo kuwaeleza viongozi hao kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imeanza kulipa fidia kwa wananchi wa eneo la Likong’o mkoani humo, ambao wamepisha mradi wa kuchakata gesi.

Mgalu, amesema jumla ya shilingi bilioni tano zimetolewa na hivyo mazungumzo yanaendelea baina ya serikali na wawekezaji kuhusu kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho kitakachochochea uchumi wa Mkoa huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live