Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mahinga azungumzia uamuzi wa Makonda kuwapigania wajane

Tue, 3 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Balozi Augustine Mahiga amesema hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kulitambua kundi la wajane katika mirathi linatakiwa kufanywa ajenda ya Kitaifa hadi Kimataifa.

Balozi Mahiga ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 3,2019 katika ofisi ya Wizara hiyo ilizopo Mji wa Serikali kata ya Mtumba jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya maombi ya muswada wa mabadiliko ya sheria ya mirathi na ndoa kutoka kwa Makonda.

Amesema wanawake wamekuwa wakipiganiwa katika masuala ya elimu, uongozi, afya, pamoja na ubunifu lakini suala la mirathi lilikuwa limesahaulika hivyo kuufanya mfumo huo kuonekana kumtenga mwanamke mjane pamoja kumuathiri mtoto.

“Nikupongeze sana Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam (Makonda) kwa hatua uliyofikia ya kulikumbuka hili kundi la wajane kwani lilikuwa limesahaulika, sasa mchakato huu ambao umeanza nao tunatakiwa kuufanya kuwa ajenda ya Kitaifa na hatimaye Kimataifa,” amesema Balozi Mahiga

Mwanadiplomasia huyo ameongeza, “katika hili, Tanzania inakuwa ni nchi ya kwanza Afrika Mashariki kulizungumzia suala hili, sasa tutalisimamia litakuwa ajenda ya Kitaifa, ajenda ya Afrika na hata Duniani.”

Awali, akiwasilisha taarifa hiyo, Makonda amesema katika mchakato wa kuandaa taarifa hiyo alikutana na wanawake wajane zaidi ya 5,000 na kugundua asilimia 80 ya wasimamizi wa mirathi hutumia mirathi kwa manufaa yao na kuiacha familia ya marehemu bila msaada.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement   ?
Amesema hali hiyo inachangiwa na vikao vya mirathi kufanyika muda mfupi baada mume kufariki wakati ambao mke bado ana majonzi au ndugu wa mume kumfukuza mwanamke asishiriki vikao, wakilenga kumdhulumu mali.

“Wapo wengine wanadiriki hata kumuambia mwanamke ndio amemuua mumewe na wanasema hayo ili wamfukuze kwenye vikao na kuchagua mtu mwingine wa kusimamia mirathi hiyo ambaye naye hafanyi alichotakiwa kukifanya, anatumia mali za marehemu kwa manufaa yake,” amesema

Hata hivyo, ameshauri sheria imtambue mke wa marehemu kama msimamizi mkuu wa mirathi  kwenye vikao mbalimbali vinavyohusu masuala ya mirathi.

amesema mwanamke ashirikishwe kwenye vikao pamoja na kubainisha adhabu ambayo itachukuliwa pindi msimamizi wa mirathi atakapoitumia kwa manufaa yake.

Chanzo: mwananchi.co.tz