Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola kesho Alhamisi anatarajia kuanza ziara Januari 9, 2020, katika Mkoa Ruvuma, Mtwara na Lindi kufuatilia masuala ya ulinzi na usalama pamoja na maagizo mbalimbali aliyoyatoa kwa vyombo vilivyopo ndani ya wizara yake.
Waziri Lugola ataanzia ziara hiyo mjini Songea mkoani Ruvuma, Januari 10,2020 Mjini Mtwara na Januari 11, 2020 Mjini Lindi ambapo katika kila Mkoa atapokelewa na mwenyeji wake ambaye ni mkuu wa mkoa na kukutana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa.
Akiwa njiani kwenda Ruvuma, Waziri Lugola amesema katika kila mkoa atafanya mkutano wa hadhara, hivyo anawataka wananchi wenye kero waje kwa wingi ili waweze kutatuliwa kero zao.
“Lengo la ziara hii ni kufuatilia utendaji kazi wa taasisi zilizopo ndani ya wizara yangu na pia kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara, ikiwa ni utaratibu ambao nilijiwekea tangu nilipoteuliwa kuiongoza wizara hii,” amesema Lugola.
Amesema ziara hiyo pia itamwezesha kufuatilia kwa ukaribu zaidi maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama ambayo ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini.
Maagizo mengine ni marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni ziondolewe.
Pia Soma
- Waziri Mpango azungumzia misaada ya wahisani kupungua Tanzania
- Card B atangaza kuhamia Nigeria, kukimbia vita ya Iran na Marekani
- Ajali ya ndege yaua watu 176 Iran
- Rais Shein aonya watakaokwamisha elimu, afya bure Zanzibar
“Pia nitawapa nafasi wananchi waulize maswali bila woga, waniambie kero zao nami nitazitatua katika mkutano huo,” amesema Lugola.
Waziri Lugola amesema katika ziara yake aliyoifanya mikoa ya Kigoma, Kagera, Arusha, Morogoro, Katavi na Rukwa, amegundua wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo hawezi kulala akiwa ofisini, lazima afanye ziara nchi nzima kuwasaidia wananchi kutatua kero zao ambapo wengi wao wakiwalalamikia na baadhi ya Polisi wakiwaonea.
“Napenda kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano yangu hiyo, wanapojitokeza itasaidia kusikiliza matatizo yao yanayowakabili, ndiyo maana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima, hii inasaidia sana kujua matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa taasisi zangu zilizopo ndani ya wizara hii,” amesema Waziri Lugola.