Kigoma. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji, amemuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmahauri ya wilaya ya Kigoma kumrejesha mara moja katika kituo chake cha kazi cha awali, dereva wa kituo cha afya Bitale, kilichoko kata ya Bitale katika halmashauri ya wilaya hiyo baada ya kubainika kuwa gari la kubeba wagonjwa kituoni hapo halina dereva.
Dk Kijaji, ametoa maelekezo hayo leo Agosti 14 alipotembelea kituo hicho cha afya kukagua ujenzi wa majengo mapya ya kituo hicho yatakayogharimu Sh400 milioni baada ya mganga mfawidhi wa kituo cha afya Bitale, Dk Norbert Nshemetse, kueleza changamoto ya upungufu wa watumishi wa kituo hicho akiwamo dereva.
Dk Nshemetse, pamoja na kumshukuru Rais John Magufuli, kwa kuwapa gari la wagonjwa (Ambulance) katika kituo hicho, amesema gari hilo halina dereva baada ya dereva wake kuhamishiwa katika ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kigoma mwezi Julai, 2018.
"Katika jambo lililonishitua ni kupata taarifa kwamba dereva aliyekuwa akiendesha gari la wagonjwa hapa kituoni amehamishwa kupelekwa kwa mkurugenzi mtendaji wakati anahitajika zaidi hapa kuliko huko kwa mkurugenzi," amesema Dk Kijaji
Amemwamwagiza Mkurugenzi Mtendaji huyo kumrejesha dereva huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja kituoni hapo ili aendelee na kazi ya kuwahudumia wagonjwa.
"Tunaposema thamani ya fedha ni pamoja na mambo haya, gari lipo lakini halina dereva. Mkurugenzi, mrejeshe dereva huyo hapa wewe tafuta dereva mwingine, mwenyekiti wa halmashauri na mkuu wa wilaya hebu lisimamie hili," ameagiza Dk Kijaji.