Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Kigwangalla afuta umiliki kitalu Green Miles Safaris, DC atoa shukrani

70396 Kitalu+pic

Wed, 7 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Dk Hamis Kigwangalla ametangaza kufuta umiliki wa kitalu cha uwindaji wa kitalii cha lake Natron (East) kilichokuwa kinamilikiwa na kampuni ya Green miles Safaris Ltd.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Jumatano Agosti 8, 2019, Waziri Kigwangalla amefuta kitalu hicho kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 38 cha sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 .

Kufutwa kwa kibali hiki, kimekuja baada ya kuwepo migogoro ya muda mrefu baina ya  vijiji 23 vya wilaya hiyo, vinaidai kampuni hiyo kiasi cha Sh329 milioni kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Licha ya madai hayo ya vijiji pia, Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilikuwa imesitisha kibali cha uwindaji wa kitalii cha kampuni hiyo kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya umiliki wa vitalu vya uwindaji.

Mkuu wa wilaya ya Longido, akizungumza na Mwananchi ameeleza kumshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa kusikiliza kilio cha wanyonge kwani kwa muda mrefu mwekezaji huyo alikuwa akilalamikiwa na wananchi.

"Tunampongeza sana Rais John Magufuli, kwa uamuzi huo kwani tumeupokea kwa furaha kubwa lakini pia tunamshukuru sana Waziri Kigwangalla kwa kazi nzuri ambayo amefanya," amesema

Pia Soma

Amesema mwekezaji huyo alikuwa akidharau Serikali wilaya ya Longido, Halmashauri na wananchi hivyo uamuzi wa kuondolewa wameupokea kwa furaha kubwa.

Mapema mwaka 2019, Naibu Kamishna wa Utalii na Biashara wa TAWA, Imani Nkuwi alisema kampuni hiyo, imeshindwa kulipa ada za kutotumia zaidi ya asilimia 40 ya mgao wa kuwinda katika vitalu.

"Kampuni hii tumeinyima huduma za kuwinda katika vitalu vyake vyote  wakati suala lao likifanyiwa kazi" alisema.

Kampuni hiyo, inamiliki vitalu wilayani Longido na katika pori la akiba la Selous  na katika siku za karibuni, imekuwa na migogoro na vijiji ilipowekeza wilayani Longido.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Longido, Wakili Jumaa Mhina, amesema ofisini yake imekuwa ikiitaka kampuni hiyo kuwa na mahusiano na vijiji na  kulipa fedha za vijiji na halmashauri bila ya mafanikio .

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Green Miles Safari Ltd, Salim Abdalah Awadhi , amekuwa akikanusha tuhuma mbalimbali dhidi ya kampuni yake, ikiwepo kudaiwa fedha na vijiji.

Chanzo: mwananchi.co.tz