Baadhi ya wazee katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele wamelalamika kutoandikishwa kwenye mpango wa kusaidia kaya masikini Tasaf 2021 wakidai kuwa walioandikishwa ni wachache ikilinganishwa na idadi iliyopo.
Akiwasilisha kero hiyo leo Jumapili Novemba 21, 2021 kwa Naibu Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Cristina Mundeme katika ziara yake ya kuimarisha chama wilayani humo, Issa Mnyakaswa (77) amedai haki haijatendeka.
“Ninachoeleza hapa ni ukweli mtupu wasinitupie lawama wahusika kwamba nadanganya, wazee wenye vigezo wengi hawajaandikishwa nikiwamo mimi,”amesema Mnyakaswa.
Amesema wale wachache walioandikishwa hadi sasa hawajaanza kupewa fedha hiyo akiongeza kuwa Tasaf inataka wajiletee maendeleo kwa kufuga kuku, mbuzi na shughuli zingine.
“Lakini kwa mwezi watapewa Sh20, 000 inakusaidia nini? unaweza kununua mbuzi, kuku au mabati mangapi? tunaomba utufikishie kero hii kwa Rais waongeze idadi ya wazee wenye vigezo na fedha,”amesema.
Akijibu hoja hiyo Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Mlele, Ignas Kikwala amesema mwaka huu walengwa ni 287 na bajeti yao itakayotolewa baada ya miezi miwili haizidi Sh40 milioni.
“Zoezi hili limefanyika ngazi ya vijiji na wanaowatambua na kuwabaini ni vijiji husika, kama kuna wazee waliachwa labda wataalamu hawakutimiza wajibu wao vizuri, niahidi kufanyia kazi,” amesema Kikwala.
Naibu Katibu Mkuu CCM Tanzania Bara, Cristina Mundeme amemuagiza ofisa maendeleo ya jamii kuhakikisha anafanya upembuzi upya wilaya nzima ili wazee waliokidhi vigezo wote waandikishwe.
“Mabilioni ya fedha Rais anatoa kwaajili ya Tasaf, ninachoomba kama wazee walivyosema Sh20, 000 wanayopewa ni ndogo nalichukua tutakwenda kuangalia upya na Serikali ili tuboreshe zaidi,”amesema Mundeme.