Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazee wa Dar walipomkaribisha Mwalimu Nyerere Mtoni kwa Chaurembo mwaka 1956

79846 Nyerere1+pic

Tue, 15 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Alasiri moja ya mwaka 1956 wazee wa Dar es Salaam wakiwa Mwembe Maulidi maeneo ya Mtoni kwa Chaurembo, Temeke jijini Dar es Salaam waliwapokea wageni tofauti na waliowazoea.

Wageni hao walikuwa ni Julius Nyerere na John Rupia ambao walikuwa na wazee wengine wa Dar es Salaam, Zubeir Mtemvu na Dosa Aziz na kujumuika na wenyeji wao chini ya Mwembe Maulidi kupata chai na vitafunwa.

Mwembe Maulidi ambao hadi sasa watu wanakula embe zake, ni mwembe kati ya miembe mingi iliyokuwa kwenye shamba la ukoo cha Chaurembo. Kwa nini imebidi kuandika kuhusu mwembe huu?

Andiko hili linatokana na picha ya kihistoria ya baadhi ya wazee wa Dar es Salaam wakiwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1956, picha ambayo imekuwa maarufu mitandaoni ikichambuliwa na kujadiliwa na watu mbalimbali.

Mwembe huu uliitwa Mwembe Maulidi kutokana na kivuli chake ambacho familia ya Chaurembo wana utamaduni wa kuutumia kukutana, kusoma Maulid au katika hafla mbalimbali zikiwamo harusi.

Kwa familia ya Chaurembo, Maulid hizi husomwa kila siku ya Sikukuu ya Idd Mosi baada ya mfungo wa Ramadhan na Idd ya Kuchinja au Idd al Adhha.

Pia Soma

Advertisement
Hata hivyo picha iliyosambaa haikupigwa siku hizo, bali ilikuwa hafla ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kujaalia mmoja kati ya familia ya Chaurembo aliyerudi Makka akitoka kutekeleza ibada ya Hijja.

Alhaji aliyerejea kutoka Makka, ni Sheikh Abdallah Idd Chaurembo na wengine waliorudi naye akiwamo Sheikh Said Hariz na Mzee Karama ambao walikuwa wakiishi Kariakoo.

Zaidi ya kumshukuru Mungu, kulikuwa na jingine, katika dini ya Kiislam inaaminika kuwa Muislam akienda kuhiji akamaliza ibada hiyo na kurejea nyumbani, mtu huyo katika siku 40, lolote la kheri analoliomba Mwenyezi Mungu huipokea dua hiyo.

Kwa hiyo wazee hawa, moja ya nia zao ilikuwa ni kuombea harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika ziwe zenye amani na mafanikio.

Sababu hasa ya kutaka amani ni wazee hawa kufahamu ukweli kwamba kipindi hicho hicho harakati za kudai uhuru nchi jirani ya Kenya hazikuwa na amani.

Wakikuyu wakiongozwa na Mzee Jomo Kenyatta walikuwa msituni wakishambuliana na Serikali ya kikoloni jambo ambalo wazee hawa hawakupenda litokee Tanganyika.

Kikundi kilichokuwa msituni kikiongozwa na Dedan Kimathi kiliingia vitani kushambuliana na kuuana na kwa ujumla maisha hasa vijijini nchini Kenya yalikuwa ya kutisha, yasiyo na amani.

Kwa kutaka uhuru wa Tanganyika upatikane kwa amani, wazee hawa wakaona umuhimu wa kumualika Nyerere ili ashuhudie dua hiyo kwa kuwa wakati huo naye alikuwa mstari wa mbele kupigania uhuru.

Dua iliyofanyika Mtoni kwa Chaurembo chini ya mwembe huo na baadaye kupigwa picha linabaki kuwa tukio la kipekee kwenye historia ya Tanganyika hasa kwa kuwa mwembe huo upo hadi leo.

Sina hakika kama mwembe huu ulipandwa ili tu uwe kwa ajili ya kusoma Maulid lakini naamini baada ya matukio ya kusoma Maulid kila mwaka mara mbili, basi mwembe huu ukajikuta ukibaki na jina la Mwembe Maulidi.

Kwa maeneo ya Mtoni kwa Chaurembo miaka hiyo kulikuwa na miembe ifuatayo; Mwembe Mashua, eneo ambalo mashua zilikuwa zikikarabatiwa.

Mwembe Popo, kutokana na uzuri wa embe zake popo walipenda kuuzingira mwembe huu.

Kulikuwa na Mwembe Pilau eneo ambalo kunapokua na shughuli chini ya mwembe huu ndipo palipotumika kupikia pilau.

Pia kulikuwa na Mwembe Kiboko, eneo ambalo wakati huo viboko walipotoka baharini walikuwa wakijipumzisha chini ya mwembe huo. Sina hakika kama miembe hii yote bado ipo ila najua ulipokuwa Mwembe Pilau kwa sasa kuna nyumba.

Katika miembe iliyokuwa ikipendwa na wazee katika shamba la kina Chaurembo, ni Mwembe Hali Mtumwa, embe zake zilikuwa tamu na usingeweza kutofautisha mbivu na mbichi, zote zilikuwa za kijani. Mwembe huu ulikuwa kilimani, embe zake ziliokotewa bondeni lakini ulikatwa wakati wa Ujenzi wa Reli ya Tazara.

Katika picha hiyo wanaonekana watoto wengi wameketi, wengi wao kama si wote ni wanafunzi wa Aljamiatul Islamiya (Sasa Shule ya Msingi Lumumba).

Kabla ya kwenda Makka, Sheikh Abdallah alikuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo lakini pia alikuwa akifundisha masomo ya dini na masomo mengine ya kawaida.

Hata hivyo baada ya tukio la chini ya Mwembe Maulidi lililomhusisha Mwalimu Nyerere, Sheikh Abdallah hakuchukua muda mrefu, aliachishwa kazi katika shule hiyo.

Sheikh Abdallah alizaliwa mwaka 1911 kijiji cha Mkamba wakati huo baba yake Mzee Idd Omar Chaurembo akiwa akida wa huko wakati wa utawala wa Mjerumani. Mzee Idd alikuwa mkazi wa Mtoni Kurasini wakati mkewe Bibi Mwanamisiki binti Mwinyibakari alikuwa mkazi wa Mtoni Kijichi.

Sheikh Abdallah alianza masomo ya dini mwaka 1919 mtaa wa Narung’ombe Kariakoo kwa Sheikh Said Pazi na pia alisoma kwa Sheikh Hussein Bin Hussein Seseme na masheikh Mohammed bin Yusuf na Athuman Said Makota.

Mwaka 1923 alianza masomo Kichwele School (sasa Uhuru Mchanganyiko) hadi darasa la sita la wakati huo na kupata Central School Leaving Certificate ambako alichaguliwa kwenda Mpwapwa kusomea ualimu lakini hakuenda badala yake alianza kazi idara ya ualimu mwaka 1932 na kuhamishiwa Tanga lakini mwaka 1934 aliacha kazi kutokana na matatizo ya macho.

Baada ya kupona matatizo ya macho, mwaka 1934 hadi 1937 alikwenda Zanzibar kusoma elimu ya dini ya kiislam kwa masheikh Suleiman Shidi, Sayid Abalhassan na Sayid Nassir lakini pia alikuwa akihudhuria darsa za ukutani za Msufini na Mbuyuni.

Mwaka 1941, Sheikh Hassan Bin Amir wa Zanzibar alihamia Dar es Salaam na hapo Sheikh Abdallah alijiunga na darasa zake na kuwa mmoja wa wanafunzi wake ambao mwaka 1950 walienda naye Rwanda, Burundi na DRC Congo kwa ajili ya kufundisha na kuhubiri Uislamu.

Ni katika kipindi hicho hicho ndipo Sheikh Abdallah alipopewa ijaza na Sheikh Hassan ya kufundisha tafsiri ya Kuran.

Kwa Dar es Salaam, Sheikh Abdallah alifundisha dini ya Kiislam katika misikiti mbalimbali kama Msikiti wa Ngazija, Rawdha ( wakati huo ukiitwa Masjid Badawiy), Msikiti wa Mtoro, Msikiti wa Makonde, Msikiti wa Kijitonyama, Msikiti wa Shadhily wakati huo pia akiwa khalifa wa twarika ya Shadhily na misikiti mingine.

Kazi hii ya ufundishaji ilikuja kama vile watu wasemavyo kwamba heri iko kwenye tumbo la shari. Kwa nini? Kwa sababu zilitokea kadhia mbili mbaya.

Kwanza palizuka tatizo la mauaji eneo la Mtoni, ndugu wa karibu wa ukoo wa Chaurembo bibi Feti binti Abdallah na mumewe waliokuwa wakiishi Mtoni kwa Azizi Ali waliuawa kikatili katika nyumba yao ambayo baadaye ilikuwa ofisi ya Tanu.

Mauaji yale yakahamia Mtoni kwa Chaurembo, na kuiandama familia ya kina Chaurembo ambako Sheikh Abdallah mara mbili alinusurika kuuawa, mara ya tatu walijaribu kumkata kwa panga na kudhani wamefanikiwa lakini panga lile lilibaki mlangoni.

Baada ya taarifa kufikishwa polisi, baba yake mdogo aitwaye Said Chaurembo alifika na gari lake na kumhamisha yeye na watoto wake wote kwenda kuishi Kariakoo kwenye nyumba yake iliyopo, Mtaa wa Kongo na Mkunguni.

Baadaye Sheikh Abdallah aliikarabati nyumba ya baba yake mzazi iliyopo Kariakoo Mtaa wa Kongo na Pemba na kuhamia hapo.

Baada ya kuhamia mjini ndipo ile kadhia ya kuachishwa kazi Al Jamiatul Muslim School ilipomkumba.

Hata hivyo kadhia hiyo ilimpa fursa mbili, kwanza alipata wasaa kufundisha masomo ya dini asubuhi nyumbani kwake Kariakoo na jioni kwenye misikiti lakini pia wanafunzi wake walioshindwa au kupata taabu kumfuata Mtoni kwa Chaurembo ikawa rahisi kwao kumpata Kariakoo.

Miongoni mwa mambo aliyopenda kuwasisitizia wanafunzi wake ni kujenga misikiti na kuweka madrasa kwa ajili ya watoto kusoma elimu ya dini.

Miongoni mwa wanafunzi wake ni Sheikh Abubakar Mwinchumu maarufu kama Maalim Dona wa msikiti wa Magomeni karibu na makaburi ya Mwinyimkuu, Sheikh Mohammed Abdallah wa Msikiti wa Mwembechai.

Wengine ni Sheikh Abdallah Mchambe wa msikiti wa Tandika, Sheikh Salum Pazi wa msikiti wa Manzese, Sheikh Mussa Salum Mahambe wa msikiti wa Temeke Kota, Sheikh Salum Mahambe ndiye baba wa Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum.

Mwingine aliyepata bahati ya kuwa mwanafunzi wa Sheikh Abdallah ni Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye mwenyewe alikiri katika moja ya Maulid za kwa Chaurembo kwamba yeye ni mwanafunzi wa Sheikh Abdallah.

Sambamba na juhudi zake za kufundisha elimu ya dini lakini pia Sheikh Abdallah alikuwa mwanajamii na mwanasiasa aliyekuwa mstari wa mbele katika harakati za uhuru wa Tanganyika.

Na ndio maana haikushangaza kwa Mwalimu Nyerere kufika Mtoni kwa Chaurembo kujumuika na wazee wa Dar es Salaam na Waislamu katika hafla iliyoambatana na dua ya kuiombea Tanganyika ipate uhuru kwa amani.

Kwa walioishi Kariakoo na Sheikh Abdallah hasa mitaa ya Kongo na Pemba wanakumbuka namna ambavyo baadhi ya wanasiasa walikuwa wakiingia na kutoka nyumbani kwake na kufanya naye vikao vya mara kwa mara.

Na hata uhuru ulipopatikana, aliendelea kuwa mwana Tanu akiwa mjumbe wa halmashauri kuu na kamati kuu ya chama hicho lakini pia Mwalimu Nyerere alimteua katika Tume ya Rais ya Kudumu ya Uchunguzi ambayo mwanasheria wake alikuwa Jaji Damian Lubuva.

Chanzo: mwananchi.co.tz