Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazee Kigoma waiangukia Serikali, manyanyaso ya familia yatajwa

Wazee Pic Data Wazee Kasulu walia unyanyasaji, waomba sheria ya kuwajali

Thu, 4 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Baadhi ya wazee wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wamelalamikia vitendo vya kunyanyaswa na baadhi ya watoto wao na kuwataka wafe ili waweze kurithi mali ikiwemo mashamba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wazee hao wakati wakipewa elimu ya uhamasishaji wa kupata chanjo ya Uviko-19 kwa wazee wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu na Kasulu Mji, elimu hiyo ilitolewa na shirika linaloshughulika na wazee HelpAge International, wamesema jamii imekuwa ikiwatenga na kushindwa kuwashirikisha katika ngazi mbalimba za kutoa maamuzi.

Mzee kutoka Rungwe mpya, Albeto Balegela amesema wazee wamekuwa wakiishi kwa shida katika jamii na familia zao kwa kutengwa na kuonekana wanausumbufu hali inayochangia kukata tama.

Amesema kama Serikali itawatungia sheria ya wazee itasaidia kupunguza vifo vingi vya wazee vinatokana na msongo wa mawazo baada ya kutengwa na jamii na wengine wanaamua kujinyonga kwasababu anakuwa ameshakata tamaa.

“Wazee tuna umuhimu wa kupata chanjo kwani tumekuwa tukiandamwa na magonjwa mbalimbali na tunakuwa hatupo salama hivyo kama tutapata chanjo itasaidia ukipata virusi vya corona utakuwa tofauti na mzee ambaye bado hajapata chanjo hiyo,”amesema Balegela

Katibu wa baraza la wazee kata ya Kalela, Gerald Tunge amesema wazee wamekuwa na changamoto mbalimbali wanazokutana zikiwemo mauaji ya wazee, wazee kuporwa mali zao na wazee kuonewa katika familia zao.

Amesema wanaomba Serikali iendelee kuelimisha umuhimu wa wazee na wazee kujua haki zao na kuweza kuzitetea, na kwamba watoto waliowazaa baadhi yao wanawanyanyasa ili wafe mapema na wao waweze kuchukua mali zao.

Ofisa ustawi wa jamii halamshauri ya wilaya ya Kasulu, Salum Masanja amesema katika kuhakikisha wazee wanapata vipaombele katika maeneo ya kutolea huduma za afya kwa kufatilia uwepo wa mabango katika maeneo hayo yanayoonyesha kumpisha mzee ili aweze kupatiwa huduma kwanza.

Amesema Serikali inajitahidi kuhakikisha dawa za wazee zinapatikana katika maeneo yote ya kupatia huduma za afya na kupatiwa huduma kwa wakati mara tu wanapofika kupatiwa huduma hizo.

Amesema halmashauri ya wilaya ya Kasulu ina jumla ya wazee 12,800 ambapo wazee zaidi ya 7,500 sawa na asilimia 60.9 tayari wameshapatiwa vitambulisho vya kuwatambulisha na kuwasaidia kupata matibabu.

Meneja mipango kutoka HelpAge Tanzania, Joseph Mbasha amesema wamezindua mpango wa kuhamasisha chanjo kwa mkoa wa Kigoma kwa wazee lengo likiwa kuunga jitihada za Serikali kupambana na ugonjwa wa virusi vya Uviko-19.

Amesema wazee wameathirika zaidi katika ugonjwa wa Uviko-19 na kwamba wao kama wadau wa wazee wakaona ni muhimu na wao kuhamasisha wazee kupitia chanjo ili waweze kuwa salama.

Amesema lengo ni kufikia angalau asilimia 80 ya wazee wote na kupitia mabaraza ya wazee ni rahisi wazee kuchanjwa lakini pia kutoa elimu kwa wazee wengine ambao bado hawajapata chanjo kuchanjwa kwa hiyari na kushawishi makundi mengine kuweza kuona umuhimu huo.

“Sisi kama shirika tumejiwekea lengo la kufikia angalau wazee 500,000 katika maeneo yote ya mradi huu ili kuweza katika sehemu inayochangia serikali na sisi tuweze kuchangia kwa kuwafikia wazee hao hata kwa asilimia 20 ya juhudi hizo kwa kundi la wazee,”amesema Mbasha.

Chanzo: mwananchidigital