Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi wenye watoto waliopotea watoa neno

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Leila Kombe, mama mzazi wa Idrissa Ally (13) akisema bado ana matumaini ya mtoto wake kupatikana, mama mdogo wa mtoto Shabaan Ngunda amesema kadri muda unavyozidi kwenda wanapoteza matumaini ya kumpata kijana wao aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha.

Idrissa, mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Princes Gate alitekwa Septemba 26, mwaka jana, saa 11 jioni kwa staili ya ‘kimafia’ akiwa anacheza na wenzake maeneo ya Tegeta na hadi jana ametimiza siku 128.

Mtoto huyo alichukuliwa na dereva mwanamume aliyekuwa katika gari aina ya Toyota IST, ambaye baada ya kuwafukuza marafiki zake alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa kuwa ni ‘spray’ na kumpulizia kisha kumuingiza kwenye gari kupitia mlango wa nyuma.

Novemba 6, mwaka jana, Shabaan akiwa na umri wa miezi sita wakati huo, alichukuliwa mchana na mtu asiyejulikana akiwa nyumbani kwa Mama Rose, Mtaa wa Ubungo Mbagala - Charambe wilayani Temeke na hadi jana ametimiza siku 87.

“Muda sasa umepita tangu Idrissa amechukuliwa, lakini bado matumaini yangu yapo kwa Mungu kwa sababu yeye ndiye anayeleta mitihani na kuiondoa. Lazima niwe na imani ya kuwa mtoto wangu atapatikana,” alisema Leila alipozungumza na Mwananchi.

Alisema anaendelea na maombi kila wakati ili mtoto wake arejee huku akiwaangukia Watanzania kutoa taarifa polisi pindi watakaposikia tetesi au kumuona.

Wakati Leila, akieleza hayo, mama mdogo wa Shaaban, Siri Nongwa alisema kadri muda unavyozidi kwenda wanapoteza matumaini ya kumpata mtoto huyo hasa ikizingatiwa umri alionao ni mdogo.

“Kwa kweli tunapoteza matumaini ya kumpata kijana wetu, maana tuliambiwa tuiachie polisi ili walifanyie kazi, lakini hadi sasa hakuna mrejesho na tukiwauliza wanatuambia tusubiri upelelezi unaendelea,” alisema.

“Tunamwachia Mungu kama atarudi tutashukuru, lakini upande wa familia matumaini hayapo kabisa na muda haurudi nyuma unazidi kwenda mbele tu.”

Shaaban alipotea baada ya mama yake, Binati Nongwa kwenda nyumbani kwa Mama Rose na baada ya kufika alimweka pembeni kisha akaagizwa kwenda kununua samaki na aliporudi hakumkuta mwanaye, lakini alipouliza alijibiwa kuwa aliondoka naye.

Kwa nyakati tofauti, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amenukuliwa akisema kuwa bado jeshi hilo halijapata taarifa zozote za mahali watoto hao walipo na kwamba, wanaendelea na upelelezi pamoja na kuwatafuta.



Chanzo: mwananchi.co.tz