Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi watakiwa kuzingatia lishe bora kwa wanafunzi

Lishe Serera Msaada wa nafaka mbalimbali ukikabidhiwa kwa walengwa

Tue, 1 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wazazi na walezi wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wametakiwa kuzingatia lishe bora kwa watoto wao ili kuboresha ustawi wao pamoja na kuongeza ufaulu shuleni kupitia upatikanaji wa chakula katika shule mbalimbali zilizopo wilayani humo.

 Akizungumza katika hafla ya kukabidhi chakula kilichotolewa na shirika World vision Tanzania kupitia mradi Ruvu Remit (AP)katika shule tisa za tarafa ya Ruvu Remit wilayani humo, Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera amesema moja ya mikakati ya kuongeza kiwango elimu ni upatikanaji wa chakula shuleni.

Shirika hilo limetoa msaada wa chakula kwa shule tisa za wilaya hiyo zikiwamo saba za msingi na mbili za sekondari.

Msaada huo wa chakula uliotolewa ni tani 50.7 za mahindi, tani 27.6 za maharage na lita 2,220 za mafuta ya kupikia ambapo chakula hicho kitatumika kuaniza mwezi Machi hadi Mei.

Dk Serera amesema mwanafunzi anapopata chakula cha kutosha shuleni hupata nguvu za kusoma kwa bidii lakini anapokabiliwa na njaa ni rahisi kushawishika kutoroka shule hali ambayo inarudisha nyuma maendeleo yake ya elimu.

Advertisement "Wenzetu Word vision Tanzania wametumia fedha nyingi kuleta chakula hiki katika shule zetu zilizopo Tarafa ya Ruvuremit ambapo ni ndani ya miezi mitatu mfululizo hivyo nawasisitiza wazazi na walezi msibweteke ni vyema mkajipanga kuhakikisha upatikanaji wa chakula shuleni unaendelea siku zote,"amesema Dk Serera.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Simanjiro, Christina Marwa amesema kupitia hali ya mabadiliko ya hali ya hewa iliyoikumba wilaya hiyo ni suala la kujifunza kwa wazazi na walezi kutoa maeneo ya mashamba ya shule ili kusaidia hupatikanaji wa chakula kwa wanafunzi pale inapotokea changamoto kama hiyo.

"Mnapotoa maeneo ya mashamba kwa ajili ya shule mnatakiwa kuwa na mkakati wa kudumu katika kuhakikisha chakula katika shule zetu kinapatikana kwani wamiliki wa shule ni wananchi hivyo inatupasa sisi sote kushirikiana kuhakikisha watoto wetu wanasoma pasipokuwa na kikwazo cha njaa,"amesema Marwa.

Amesisitiza kuwa endapo maeneo ya mashamba ya shule yakapatikana watakaokuwa wanalima ni wazazi kwa kutenga siku moja ndani ya wiki kwa ajili ya kulima lengo ni kuhakikisha watoto shuleni wanakuwa na ustawi bora pasipokuwa na kikwazo cha njaa.

Mwezeshaji wa mradi Ruvuremit (AP) wa shirika la World Vision Tanzania, Aizack Mwaijande amesema chakula hicho watatoa ndani ya miezi mitatu ambapo kitagharimu zaidi ya Sh148.2 milioni kwa watoto 3696.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ngage, Evans Mtalo ni mmoja wa wanufaika, pia amelishukuru shirika hilo kwani limewamewasaidia katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji hapo shuleni unaozingatia upatikanaji wa chakula kwani kwa kipindi cha mchana watoto hawawezi kusoma na wanakuwa wanalegea kutokana na kukabiliwa na njaa.

"Watoto wanashindwa kupokea vipindi vya mchana kwani asubuhi huwa na nguvu lakini kadri muda unavyoenda ndipo kasi ya kujifunza inapungua hivyo tunawaomba wazazi wasibweteke bali tujipange suala la upatikanaji chakula shuleni liwe endelevu,"amesema Mwalimu mkuu huyo.

Baadhi ya wazazi wamesema hapo awali walikuwa wanatoa chakula shuleni kwa ajili ya watoto wao lakini kwa bahati mbaya uchumi wao uliyumba kutokana na janga la ukame lililosababisha mifugo kufa na kupelekea kushindwa kuendelea na zoezi hilo.

Wakisimulia adha waliyokuwa wanapata baadhi ya wanafunzi shuleni ni kuchoka na kusinzia hali inayowapelekea kutoroka vipindi vya shule kutokana na njaa wanayohisi katika nyakati za mchana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live