Zuwena Said mkazi wa Muriet, jijini Arusha ameiomba serikali kumsaidia ili amzike mtoto wake Ally Hamad (30) baada ya kuibuka mgogoro wa wapi pa kumzika kati yake na mzazi mwenzake aliyedai kwamba kama vipi mwili waukate yeye achukue miguu na baba achukue kichwa akazike.
Ally (Pichani) alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mount Meru, ambapo baba mzazi anataka mtoto wake akamzike mkoani Singida alipozikwa Babu wa marehemu.
Zuwena amesema kuwa, mzazi mwenzake aliwatelekeza wakati mtoto Ally akiwa na umri wa miaka 5 na hakumhudumia kwa chochote na hata kipindi anaumwa baba huyo bado hakutoa chochote.
Hata hivyo, mara baada ya kijana huyo kufariki dunia ndipo baba huyo amejitokeza na kudai apatiwe mwili huo akazike na si mwanamke kwenda kumzika kwao la sivyo waugawane mwili vipande kila mtu akazike kivyake.
Baba wa marehemu Ally aitwaye Hamad Juma alimtekeleza mzazi mwenzake wakati mtoto akiwa na umri wa miaka mitatu pasi na matunzo yoyote lakini ghafla ameibuka mara baada ya taarifa za kifo na tayari amekata kibali cha kuusafirisha mwili huo kuelekea Singida kwa ajili ya maziko huku mwanamke naye akitaka azike kwao Arusha.
Zuwena anaiomba Serikali na Dawati la Jinsia kuangalia suala hilo kwa upana ili kulipatia ufumbuzi kwani anachohitaji ni mwanaye kupumzishwa kwa Amani kwenye nyumba yake ya milele.
Baba huyo amesema lengo lake ilikuwa ni kwenda kumzika mwanaye Singida lakini kutokana na mgogoro huo amedai hatoshiriki tena kwani amechukia hivyo atabaki kuwa ni baba mlezi.