Asilimia 57 ya wanafunzi waliopaswa kuanza kidato cha kwanza katika Kata ya Chitete iliyopo Wilaya ya Momba mkoani Songwe hawajaripoti shule licha ya shule zote nchini kufunguliwa tangu Januari 8, 2024.
Kutokana na changamoto hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda ametoa siku saba kwa uongozi wa Wilaya ya Momba kufanya msako wa nyumba kwa nyumba katika Kata ya Naming’ong’o na Chitete na kuwachukulia hatua wazazi au walezi ambao watoto wao hawajaripoti shule.
Seneda ametoa maagizo hayo leo, Alhamisi Januari 18, 2024 wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa miradi ya elimu na nyumba ya Mkuu wa Wilaya na kubaini asilimia 57 ya wanafunzi hawajaripoti shule kwa kisingizio cha wazazi kutowanunulia sare za shule.
Seneda amesema katika Kata ya Chitete wanafunzi 284 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza shule ya sekondari Naming’ong’o, wanafunzi 78 ndio walioripoti sawa na asilimia 43 kitendo ambacho kimemshangaza.
Kutokana na hali hiyo Seneda amemuagiza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri na Katibu Tawala wa Wilaya kusimamia shughuli ya kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanaripoti hata wakiwa hawana sare.
Akiwa katika shule mpya ya Sekondari Naming’ong’o iliyojengwa kwa Sh583.1 milioni, ameshangaa kuona wanafunzi 35 kati ya 78 pekee ndio wameripoti, hali ambayo ameeleza inadidimiza taaluma ya elimu ya kutoa maelekezo ya msako wa nyumba kwa nyumba kuwabaini na kuchukua hatua kwa wazazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Momba, Manoza Fabian amesema wanafunzi wengi hawajaripoti kutokana na wazazi na walezi kuwatumikisha kwenye kilimo na mifugo na watakwenda kutekeleza agizo hilo mara moja.
“Tumepokea agizo hilo kuhakikisha watoto wote wanaripoti shule, wazazi na walezi watakaowatorosha watoto na kuwatumikisha mashambani au kuchunga mifugo watachukuliwa hatua za kisheria,” amesema Fabian.
Naye Ofisa Elimu Sekondari, Frorence Haule amesema kwa upande wa sekondari ya Chitete, wanafunzi 206 hawajaripoti huku Naming’ong’o wanafunzi 43 jumla ya wanafunzi 249 hawajaripoti, jambo ambalo wazazi watakaobainika kuwa kikwazo watachukuliwa hatua kali ili kuhakikisha ndoto za watoto wao zinatimia.
Mmoja wa wazazi hao, Juma Sinyangwe, mkazi wa Kata ya Naming’ong’o amesema changamoto baadhi ya walimu hawawaruhusu wanafunzi kwenda bila kuvaa sare za shule kwa kukinzana na agizo la Serikali.