MKUU wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Nurudin Babu, amesema hatosita kuwaburuza kortini, wazazi na walezi wanaotoka jamii za kifugaji ambao watakaidi amri halali ya kuwaandikisha shule watoto wenye umri wa kuanza darasa la kwanza mwaka ujao.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo, waliojitokeza katika mahafali ya saba ya Shule ya Sekondari ya Tingatinga iliyopo Tarafa ya Enduimet.
Alisema imebainika kuwa watoto wengi wanaoanza shule hiyo malengo yao hayatimii kutokana na utoro na wengine kuozwa katika umri mdogo.
“Utoro huu unatokana na watoto kuacha masomo na kukimbilia nchi jirani ya Kenya, kwa ajili ya kufanya kazi. Mtoto yeyote mwenye umri chini ya miaka 18 anayesoma ni marufuku kuacha masomo, ila ambaye hayupo kwenye umri wa masomo, akitaka kwenda popote aende,” alisema Babu.
Kuhusu matatizo yanayoikabili shule hiyo ikiwamo ukosefu wa uzio, Babu alisema atafanya mazungmzo na menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, kuwaomba fedha za ujirani mwema zisaidie ujenzi wa shule hiyo iliyopo kwenye hifadhi na mapito ya wanyamapori.
Awali, Mkuu wa Shule hiyo, Pantaleo Paresso, alisema wahitimu hao walianza masomo wakiwa 297, lakini wanaohitimu 271, huku sababu kubwa ikiwa ni utoro na wengine kuhama.
"Hali ya ufaulu kwa miaka miwili ya nyuma ilikuwa nzuri. Mwaka 2019 tulifaulisha kwa asilimia 87, 2020 sawa na asilimia 94, na tunatarajia mwaka huu kufaulisha kwa asilimia 100,"alisema Paresso.
Alisema shule hiyo inatarajia kutoa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), baada ya jengo na vifaa kukamilika kwa gharama ya Sh. milioni 103, lakini tatizo lililopo hakuna mwalimu wa TEHAMA.
Asilimia 100 ya Shule za sekondari za wilayani hiyo ni za bweni, lakini hazina uzio na mazingira ya shule hizo ni magumu.
Mbunge wa Longido, Dk. Steven Kiruswa, aliwahi kusema katika jitihada za kuhakikisha uzio unapatikana kwa shule hizo, amepata mbegu ya mchongoma ya muda mfupi itakayoweza kuoteshwa kuzunguka mipaka ya shule ili kuwa na uzio wakati serikali ikijipanga kujenga uzio imara.