Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi wajenga mabweni, wawazuia watoto wao kuyatumia

36600 Pic+mabweni Wazazi wajenga mabweni, wawazuia watoto wao kuyatumia

Mon, 14 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nyang’hwale. Wakati wazazi katika maeneo mengi nchini wakitaka mabweni kwa watoto wao wa kike wanaosoma shule za umma, baadhi ya wazazi wa Wilaya ya Nyanghwale, Geita hawataki.

Mkuu wa wilaya hiyo, Hamimu Gwiyama amesema hiyo ni miongoni mwa sababu za wanafunzi kukosa muda wa kutosha wa kujisomea na hivyo kufanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa.

“Wapo tayari kuchangia ujenzi wa mabweni katika shule zilizoko kwenye maeneo yao lakini hawataki watoto wao waishi wala kukaa kwenye mabweni,” alisema Gwiyama.

Wilaya ya Nyang’wale ina jumla ya shule 10 za sekondari, nane kati ya hizo zina mabweni yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi.

Gwiyama alisema kutokana na umbali mrefu wa kutoka na kwenda shule, baadhi ya wanafunzi hukata tamaa na kuanza tabia ya utoro huku wa kike wakianza kujihusisha na mapenzi na waendesha pikipiki ili kupata fadhila ya lifti na mwishowe hukatisha masomo kwa kupata ujauzito.

Kwa mujibu wa takwimu za idara ya elimu mkoani Geita, jumla ya wanafunzi 160 walikatisha masomo kwa kupata ujauzito wilayani Nyang’wale katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, hii ikiwa ni wastani wa wanafunzi 53 kila mwaka.

Wilaya hiyo ina wanafunzi 6,756 katika shule zake za sekondari, kati ya hao 3,391 wakiwa wa kike na 3,365 ni wavulana. Lakini kwa mujibu wa mkuu wa wilaya, wanaoishi bwenini hawazidi 1,000.

“Kutokana na wazazi wa Nyang’wale kukataa watoto wao kuishi katika mabweni, wenzao kutoka wilaya na mikoa mingine huchangamkia fursa hiyo kwa kuwaombea watoto wao nafasi za bweni katika shule za Wilaya ya Nyang’wale,” alisema Gwiyama.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyang’hwale, John Mabere alisema bweni la wanafunzi wa kike shule hapo lenye uwezo wa kuishi wanafunzi 300 hivi sasa linakaliwa na wanafunzi 100 pekee ambao wengi wao wanatoka nje ya wilaya hiyo.

“Wakati mabweni yako tupu, wapo baadhi ya wanafunzi wanatembea umbali wa kilomita 14 kwenda na kurudi shuleni lakini wazazi wao wamegoma wasiishi bwenini,” alisema Mabere.

Wazazi wa wanafunzi wanaoishi bwenini wanatakiwa kuchangia gharama ya chakula kwa kutoa madebe matatu ya mahindi, kilo 25 za mchele na 25 za maharagwe, mazao ambayo yanalimwa na kuvunwa kwa wingi na wakazi wa wilaya hiyo.

Diwani wa Nyag’hwale, Agatha Athuman alitaja uelewa na mwamko mdogo kuhusu elimu kuwa miongoni mwa sababu za baadhi ya wazazi wilayani humo kutotilia maanani elimu kwa watoto wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’wale (DED), Mariam Chaurembo alisema ofisi yake itaitisha mikutano ya wazazi wa shule zote wilayani humo kujadili maendeleo ya elimu na matumizi ya mabweni itakuwa miongoni mwa ajenda kuu.

Mmoja wazazi, Michael Kapaya alisema moja ya sababu ya kukataa watoto kukaa bweni ni ili kuwatumia katika uzalishaji mali ikiwamo kilimo na ufugaji.

“Sasa mtoto akienda kuishi huko shuleni nani atasaidia kazi za nyumbani, shambani na kuchunga mifugo? Watoto wa kiume wanapokwenda shambani au machungani, wenzao wa kike husalia nyumbani kufanya kazi za nyumbani,” alisema Kapaya.



Chanzo: mwananchi.co.tz