Wazazi Mkoa wa Shinyanga wameiomba serikali kuwaruhusu watoto kubaki nyumbani siku za mapumziko ili kuwapeleka katika maombi na Madrasa hali itakayosaidia kuondokana na matukio ya ukatili (Ubakaji na ulawiti).
Akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ushauri wa Mkoa (RCC) kilichofanyika Februari 14,2023 ,Mwenyekiti msaidizi wa amani Mkoa,Sheikh Khalfan Ally,amesema idadi kubwa ya watoto hawapati malezi ya kiroho hali inayosababishwa na kutumia muda mwingi wakiwa shuleni.
Sheikh Ally amesema kuwa wazazi hawapati wakati wa kuwalea watoto wao kitabia hali inayosababisha kuporomoka kwa maadili sambamba na kuwepo kwa vitendo vya ulawiti.
"Wanafunzi wengi wanakaa mudaa mrefu sana shuleni kiasi kwamba tunakosa nafasi ya kumlea mtoto kitabia,halafu utakuta walimu wanalalamika wazazi hawatusaidii,tunakosa muda wa kuwalea watoto wetu kitabia kwa sababu ya masomo ya ziada(Tuition)",amesema Sheikh Salum.
Kwa upande wake Afisa elimu Mkoa wa Shinyanga Dafroza Ndalichako amesema amepokea ushauri na maombi kutoka kwa wazazi ya kuwaruhusu watoto mapema siku za mapumziko ambapo amebainisha kuwa katika shule za Mkoa huo kwa wiki kuna vipindi viwili vya dini huku akiwataka walimu wa dini kutoa elimu kwa wanafunzi hao.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Dkt.Yahaya Nawanda amemtaka Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Leornad Nyandahu kufuatilia na kuhakikisha kesi 28 za ubakaji zinafikishwa mahakamani na kutolewa hukumu.