Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi waelekeza watoto wao kuandika ‘madudu’ mitihani

37644 WAZAZIPIC Wazazi waelekeza watoto wao kuandika ‘madudu’ mitihani

Tue, 22 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ruangwa. Licha ya Serikali kujenga shule za kata kwa wingi ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari, wazazi wilayani Ruangwa mkoani Lindi wamelalamikiwa kuwajengea watoto wao mazingira ya kufeli mitihani ya darasa la saba ili wasiendelee na shule badala yake waolewe.

Hayo yalibainika wakati wa mdahalo wa wanafunzi kuhusu mila na desturi zinazochochea mimba za utotoni ulioandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), wilayani humo.

Kwa nyakati tofauti wanafunzi hao walisema baadhi ya wazazi huwalazimisha kukataa shule au kuwashauri wakosee majibu ya mitihani ya darasa la saba ili iwe rahisi kwao kuolewa.

“Kuna mwenzetu mmoja alikuwa na akili sana, lakini matokeo yalipotoka hakufaulu kujiunga na sekondari, tulipomuuliza kulikoni alisema mama yake alimwambia aandike 0000 ili afeli na aolewe,” alisema Zahara Chigope, mwanafunzi wa kidato cha nne Sekondari ya Nambilanje.

Nasma Kumkana alisema wazazi kuwashawishi wanafunzi kufeli ni tatizo kubwa na wanalisikia kutoka kwa wanafunzi wenzao.

“Siyo hivyo tu, hata baadhi ya wazazi tunawasikia wanasema bora mtoto afeli kwa sababu hawana fedha za kumhudumia atakapoingia sekondari, hata wakiambiwa elimu ni bure watasema hawana fedha za sare za shule,” alisema Nasma.

Alisema utaratibu huo unaambatana na ule wa baadhi ya wazazi kuwataka watoto wao watafute mboga kwa jasho lao.

“Hii ina maana kwamba mama anamwambia mtoto leo zamu yako kutafuta mboga, kwa maana nyingine mtoto wa kike anapewa ruhusa ya kuwa na mwanamume ili apate fedha ya kusaidia familia.”

Akizungumzia suala hilo, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nambilanje, Charles Chitawala alisema tatizo hilo ni kubwa kwa kata ya Nambilanje na maeneo mengine ya Ruangwa.

“Sisi kama viongozi suala hilo linatuudhi inabidi tutoe elimu ili tabia hizo waziache. Ilifikia mahali ikabidi tuitishe vikao vya wazazi na wazazi wajaze mikataba,” alisema Chitawala.

Alisema mwaka jana wazazi walijaza mikataba na kukubaliana kuwa iwapo mzazi atabainika kumshauri au kumlazimisha mwanafunzi kufeli atachukuliwa hatua za kisheria.

Chitawala alisema mikataba hiyo ilitolewa na uongozi wa halmashauri ya wilaya na kusainiwa na wazazi wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba.

Mratibu wa elimu kata ya Nambilanje, Lista Mziwanda alisema wazazi kuwalazimisha wanafunzi kuandika ‘madudu’ kwenye mitihani ya Taifa ni tatizo la muda mrefu, lakini hawana takwimu rasmi.

“Tulibaini mambo hayo baada ya kuwabana wanafunzi ambao tuliwategemea kufaulu lakini hawakufaulu. Ukikaa na mtoto vizuri anakuambia ukweli kuwa alilazimishwa na mama,” alisema.

Mmoja wa wazazi, Esha Chigope alisema kuwa kuna mzazi mwenzao aliyekiri kumshauri mtoto wake kuandika 1111 ili afeli mtihani wa darasa la saba.

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilu alionya kuwa watawachukulia hatua wazazi wanaowarubuni wanafunzi kufeli na kwamba mwamko wa elimu kwa ukanda wa kusini hasa vijiji vya Nambilanje, Namichiga, Nachienjele na Nanjaro bado ni ndogo na inahitajika elimu ya kutosha kuukwamua.



Chanzo: mwananchi.co.tz