Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi wa watoto wenye ulemavu wapewa neno

Cf4779abee3bc5d6c46333aa90e24da2.jpeg Wazazi wa watoto wenye ulemavu wapewa neno

Thu, 19 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZAZI na walezi wa watoto wenye ulemavu wameonywa kuwanyanyasa na kuwanyima haki za msingi watoto wao ikiwemo elimu kwani ulemavu huo hawakupata kwa kujitakia na wala watoto hao si mikosi katika familia au jamii wanayoishi.

Ushauri huo ulitolewa na Mwezeshaji wa Elimu Jumuishi kuhusu ulemavu na eenye ulemavu Wilaya ya Dodoma na Bahi, Fortunatus Raphael wakati akitoa mafunzo kwa asasi za kiraia juu ya ushawishi na utetezi kwa watu wenye ulemavu wilayani Bahi na Dodoma katika Mkoa wa Dodoma.

Raphael alisema wazazi na walezi wanatakiwa kuachana na mila hizo potofu ambazo zinachangia kuwakandamiza watoto hao na kuwanyima haki za msingi kama vile watoto hao walizaliwa hivyo kwa kujitakia au watoto hao mikosi katika familia zao.

“Wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu wanatakiwa kuachana na mila potofu ya kuona watoto hao ni mikosi katika familia zao na hivyo kuwanyima haki zao za kimsingi wanazostahili,” alisema.

Raphael alisema mila na imani potofu hizo zimejengeka miongoni mwa wazazi, walezi na jamii kwamba watoto hao ni mikosi katika familia, ambayo imesababisha watoto wenye ulemavu kukosa haki zao za kimsingi kama watoto wengine, jambo ambalo si kweli.

Alisema kutokana na kujengeka kwa imani hiyo potofu bado wazazi na walezi wamekuwa wakiwanyima haki ya msingi ya kupata elimu, badala yake wamekuwa wakiwaficha na kuwafungia majumbani badala ya kuwapeleka shuleni ambako wangeweza kujifunza pamoja na wenzao na wakafaulu masomo na hivyo kuwapunguzia ugumu wa maisha.

Awali wanafunzi wa Shule ya Msingi Ibihwa wilayani Bahi mkoani Dodoma, wameiomba serikali kuchukua hatua za kisheria kwa wazazi na walezi wanaozima ndoto ya kujikomboa na umasikini kwa mototo mwenye ulemavu.

Andrea Ladislai (15) alisema watoto wenye ulemavu wanafanyiwa ukandamizaji na wazazi, walezi na hata jamii inayowazunguka kwa kuwaona kwamba watoto hao hawastahili kupatiwa haki zao za msingi kama watoto wengine.

Mathonya Choda (14) alisema: “Sisi kama watoto wa wilaya ya Bahi mkoani Dodoma tunaiomba serikali kuingilia kati suala la ukandamizaji wanaofanyiwa watoto wenzetu wenye ulemavu ambalo limekuwa likizimisha ndoto zao za kujikomboa na umasikini walionao.”

Naye Mratibu wa Elimu Jumuishi katika Wilaya ya Bahi na Dodoma kutoka Kanisa la Free Pentecost Church of Tanzania, Jane Mgidange, alisema bado kuna majengo ya serikali yasiyo rafiki kwa watu wenye ulemavu hali ambayo inayoonesha unyimaji wa haki zao kwa kundi hilo.

Chanzo: habarileo.co.tz