Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi Mbeya wajipanga, wabakaji imekula kwao

Wed, 27 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Kutokana na kuibuka kwa matukio ya ubakaji na ulawiti  kwa watoto wenye umri wa miaka kuanzia mitatu hadi  14 katika Kitongoji cha Mageuzi, Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi, Mbeya, wazazi na walezi wameanzisha mkakati  wa kuwapeleka  na kuwarejesha nyumbani wanafunzi baada ya muda wa masomo

Wakizungumza na Mwananchi Leo Februali 27, 2019, wamesema wamelazimika kuweka  mkakati huo kwa sababu matukio hayo yamewaathiri kwa kiwango kikubwa.

Mzazi, Halima Ally anasema wamelazimika kusitisha shughuli zao asubuhi na kuhakikisha watoto wanafikishwa shule wakiwa Salama.

"Kimsingi, kabla ya  matukio haya kuibuka, wazazi tulisahau majukumu yetu kwa watoto sasa tumeamka na kutambua nini cha kufanya katika kutunza na kulinda watoto ili wapate elimu bora na matunzo pia,” amesema mama huyo.

Lusajo John, mkazi wa Nsalala anasema ili kukabiliana na matukio hayo, umefika wakati kwa wazazi kushirikiana na walimu kufuatilia mienendo ya watoto wao wawapo shuleni na nje ya hapo.

Diwani wa Kata ya Nsalala, Kissman Mwangomale, anasema mikakati hiyo ya wananchi ni maagizo yaliyotolewa  kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kitongoji hicho baada ya watoto watatu kubakwa na mmoja kulawitiwa.

Anasema kuwa walilazimika kuwaagiza wazazi na walezi baada ya kubaini wengine  hawatambui majukumu ya kutunza na kulinda familia zao .

"Tulipoona matukio hayo yameshamiri tukafuatilia na kugundua watoto wengi wanakosa usimamizi wa karibu na wazazi na hivyo hata watu wenye nia mbaya wanawadhuru na ndio tukaagiza kila mzazi anapokwenda kama ana mtoto mdogo ahakikishe anakuwa naye sambasamba na wanaosoma wafikishwe shuleni" anasema.

 

Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Nsalala, Christian Mwaisela alisema tangu viongozi watoe maagizo kwa wazazi, mwitikio wa kupeleka watoto shule umekuwa mkubwa na hatuna tukio lingine la ubakaji lililoriporiwa.

Mwalimu wa Shule ya msingi Mageuzi kitongoji cha Mageuzi, Friday Minja, anasema kufuatia matukio hayo wanaangalia namna ya kupunguza muda wa masomo ya ziada kwa wanafunzi hususan wa darasa la saba na kwamba kati ya waliofanyiwa kitendo hicho mmoja ni mwanafunzi wa shule hiyo.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz