Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi Dar walivyoonyesha mwitikio uandikishaji darasa la kwanza

90907 Pic+wazazi

Mon, 6 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku ya kwanza ya upokeaji wa wanafunzi wanaoanza masomo ya darasa la kwanza nchini Tanzania, katika baadhi ya shule za Jiji la Dar es Salaam imeonyesha mwitikio mkubwa kutoka kwa wazazi na walezi.

Leo Jumatatu Januari 6, 2020  wazazi na walezi wameonekana wakiwapeleka shule watoto wao ambapo mama wa Faudhia Ramadhani aliyefanikiwa kupata nafasi shule ya msingi Makuburi Dar es Salaam amesema pamoja na mwamko huo, wazazi na walezi wanatakiwa kuongeza umakini kwa watoto wanaoanza masomo hayo.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mabibo, iliyopo Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, Hussein Mlela Dady amesema hadi saa 2:00 asubuhi ya leo tayari ameshasajili zaidi ya watoto 20, wanaofanya idadi kufikia 110.

“Hawa 110 tutawagawanya katika madarasa mawili ya mkondo A (55) na B(55), usajili unaendelea hadi Machi 31 kwa hiyo hadi jioni tunaweza kuwa na 120 au 130,” alisema huku akifafanua kuwa shule itawapokea wanafunzi katika mikondo hiyo miwili bila kujali idadi yao.

“Huwezi kuwakataa watoto wakiletwa, madarasa tunayo mengine ila yanahitaji ukarabati tu.”

Mwandishi wa Mwananchi ameshuhudia msafara wa wazazi wakiwa wameongozana na watoto wao katika Shule ya Msingi Tabata, Mabibo na Makuburi za Dar es Salaam. Idadi kubwa ni akina mama na watoto wakiwa kwenye sare za shule wengine mavazi ya kawaida.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Mlundikano wa wazazi na walezi umeonekana katika shule ya msingi Mabibo, wakisubiri usajili na wengine kupangiwa mkondo, hali iliyoonekana pia katika shule ya Msingi Makuburi ambako uhakiki wa majina uliendelea kabla ya kuelekea darasani wakati huo huo.

“Nimekuja peke yangu, mama hayupo nyumbani,” ndiyo maneno aliyoweza kuzungumza mwanafunzi David Burugu aliyekwenda bila mzazi shuleni hapo Makuburi. Hakueleza anaishi na nani. Hatua hiyo ilibainika baada ya David Burugu kuonekana peke yake wakati wanafunzi na wazazi wakipangiwa mkondo.

Katika shule ya msingi Liwiti iliyopo Tabata Dar es Salaam wazazi wamewapeleka watoto wao kuandikishwa.

Tofauti na shule nyingine za Tabata Jica na Mtambani ambako watoto wameripoti na kuingia madarasani, hali ni tofauti katika shule ya Liwiti ambako bado walimu walikuwa wanaandikisha wanafunzi hao.

Walimu wa shule hiyo wamekataa kuzungumza chochote kuhusu uandikishaji huo na kama vyumba vya madarasa vinatosha badala yake wamemtaka mwandishi kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala ili kupata taarifa hizo.

Hata hivyo, wazazi wa wanafunzi wamesema wamewapeleka watoto wao katika shule hiyo kwa sababu iko karibu na makazi yao na kwamba ina walimu wazuri wa kufundisha watoto wao.

"Hii ni moja ya shule bora za serikali hapa Tabata, nina mtoto mwingine anasoma hapa, naona maendeleo yake ni mazuri, nimeamua kumleta na huyu mwingine," amesema Joseph Maneno, mzazi wa mwanafunzi.

Kwa upande wake, Mwanahamisi Mohammed amesema amechelewa kumwandikisha mwanaye kwa sababu alikuwa safarini. Hata hivyo, amesema amefanikiwa kupata nafasi katika shule hiyo ya msingi.

Mwananchi limetembelea shule ya Liwiti na kubaini wanafunzi wengi wa darasa la kwanza wakiwa wameripoti na kuwekwa kwenye vyumba viwili vya madarasa.

Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi hao wamevaa nguo za kawaida wakati wenzao wakiwa wamevaa sare za shule. Wamedai kwamba bado wazazi wao hawajawanunulia sare hizo.

"Mama amesema nije shule kesho ataninunulia uniform na viatu," amesema mwanafunzi mmoja, Feisal Abeid.

Chanzo: mwananchi.co.tz