Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawili wahofiwa kufariki lori likilipuka Butiama

Lori Ajali Kahama.png Wawili wahofiwa kufariki lori likilipuka Butiama

Mon, 4 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu wawili wanahofiwa kufariki dunia baada ya lori walilokuwemo kupoteza muelekeo, kuingia mtoni kisha kulipuka katika eneo la Makutano ya barabara ya Mwanza- Musoma - Tarime.

Tukio hilo limetokea leo Jumatatu Desemba 4, 2023 saa 12 asubuhi katika eneo la Makutano wilayani Butiama.

Watu hao ambao ni dereva na utingo wake bado hawajajulikana majina yao na uelekeo wao kutokana na kushindwa kutoka nje baada ya gari kutumbukia mtoni na kulipuka.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema gari hilo ambalo bado namba zake hazijajulikana lilikuwa na tela namba T828 BEJ.

"Bado hatujajua kulikuwa na watu wangapi na pia hatujajua kama hao wawili walioonekana wamefariki au la tunataka tuone haya mabaki ili tuweze kujua zaidi," amesema

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase amesema gari hilo lilikuwa linatoka uelekeo wa Mkoa wa Mwanza na kwamba hadi sasa haijajulikana lilikuwa linaelekea wapi.

Amesema kwa mujibu wa uchunguzi wa awali wamebaini kuwepo kwa mapipa ambayo yanadhaniwa kuwa na kemikali ingawa haijajulikana kulikuwa na kemikali za aina gani na zilikuwa zinapelekwa wapi.

"Hizi kemilali ni kama za kwenye migodi, tunafanya mawasiliano na migodi iliyopa hapa Mara ili tuweze kujua zaidi mzigo ulikuwa unaelekea wapi na akinanani walikuwepo kwenye gari," amesema

"Kwa mujibu wa watu walioshuhudia, hili gari lilikuwa linatoka barabara ya Mwanza likafika hapo kwenye mteremko mwendo ukaongezeka wakaonekana watu wawili yaani dereva na abiria wakipungia watu kuashiria wapishe njia ndipo likapita na kuingia kwenye mto," ameongeza Kamanda Morcase

Baadhi ya mashuhuda wamesema tukio limetokea saa 12 asubuhi ambapo gari hilo lilishindwa kupita kwenye mzunguko ( roundabout) na kuelekea mtoni kabla ya kulipuka.

"Mimi nilikuwa hapo kwangu ghafla nikaona gari linakuja kwa kasi sana likaingia mtoni ndani ya sekunde mbili likalipuka na hakuna mtu aliyeweza kutoka kwenye gari," amesema Halfan Yusuph mkazi wa Makutano

"Nadhani gari lilifeli breki likaelekea mtoni na kitendo cha kutua tu mtoni kukatokea mlipuko mkubwa sana, sina uhakika kama waliokuwemo wapo hai maana hapo ni mabaki tu ya gari ndo yanaonekana," ameongeza Anna Francis

Chanzo: www.tanzaniaweb.live