Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawili wafa kwa kugongwa na lori lililobeba wahamiaji haramu

RPC NJOMBE HAMIS ISSA.jpeg Kamanda Hamisi Issah

Mon, 10 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu wawili wamefariki dunia baada ya gari ndogo waliyokuwa wamepanda kugongwa na lori linalodaiwa kusafirisha wahamiaji haramu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issah alisema hayo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 9:00 usiku katika Kijiji cha Mng’elenge wilayani Wanging’ombe.

Alidai kuwa wahamiaji haramu 100 kutoka Ethiopia wamenusurika kifo katika ajali hiyo baada ya lori lililokuwa limewabeba kugongana na gari ndogo Toyota Mark X kisha watu wawili waliokuwa kwenye gari ndogo kupoteza maisha.

“Kulitokea ajali kati ya lori na gari moja aina ya Mark X, wale waliokuwa kwenye gari dogo walifariki dunia wote,” alisema Issah.

Kamishina wa Uhamiaji Njombe, Vicent Haule alisema walifanya msako shambani baada ya kupata taarifa kwa wananchi waliowaona wahamiaji hao waliokuwa wakijificha baada ya kupona kwenye ajali.

Alisema jeshi hilo la uhamiaji limefanikiwa kuwakamata raia 63 wa kigeni waliokuwa wakielekea Afrika Kusini.

“Hawa raia wametokea Nairobi wakafika Mombasa na kuingilia Tanga, tumeshawapata 63, bado wengine kama 40 wanaendelea kutafutwa, tuombe wananchi mtakapoona raia kama hawa Waethiopia mtupe taarifa,” alisema Vicent Haule.

Mkazi wa Wilaya ya Wanging’ombe, Tegemea Mahenge alisema walisikia mlio wa ajali usiku na walipofika wakaona watu waliokuwa kwenye gari ndogo mmoja amefariki, huku wahamiaji haramu wakijificha shambani. Diwani wa Wanging’ombe, Geofrey Nyagawa aliwataka wananchi kujiepusha na biashara chafu kwa kuwa athari zake ni kubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live