Miili ya watu wawili kati ya 17 waliofariki kwenye ajali Wilayani Korogwe imeagwa katika Hospitali ya Magunga na kusafirishwa hadi Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya taratibu za mazishi huku miili iliyosalia ikitarajiwa kuagwa hapo kesho.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga wa Omary Mgumba amesema sababu ya kuaga miili hiyo leoleo ni kutokana na miili hiyo kuharibika vibaya kutokana na ajali iliyotokea, miili iliyoagwa ni wa Festo Mwambugu na Eluminata Silayo ambao walikuwa kwenye fuso ambapo mmoja unapelekwa Mwanga na mwingine Himo Mkoani Kilimanjaro.
“Tumeaga leo kutokana na ndugu wa marehemu kuhitaji miili hiyo kwa ajlili ya mazishi kutokana na kwamba imeharibika sana hivyo miili mingine iliyobaki itaagwa kesho,” amesema Mgunda.
Aidha, Mgumba amewasimamisha kazi Mganga Mkuu wa Wilaya ya Korogwe (DMO), Dk. Salma Swedi na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Magunga Korogwe Dk. Heri Kiwale kupisha uchunguzi wa sababu zilizowapelekea kuchelewa kufika eneo la tukio.
Aidha, Mgunda ameunda kamati ya uchunguzi kupitia kwa katibu tawala wa mkoa huo na kuipa siku 14 kufanya uchunguzi huo kwa kina na kutoa majibu kwa nini madaktari hao walichelewa kufika eneo la ajali iliyotokea saa 4:30 usiku na wao wakafika saa 10 kasoro usiku.
"Serikali imekasirishwa na kitendo hichi, wananchi wameona, waathirika wameona na wameumia, hii haikubariki. Madaktari hawa watapumzika siku 14 kupisha uchunguzi huo kwa nini walifanya hivyo," amesema Mgumba.