Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wavuvi 51 wasalimisha zana haramu Rorya, wapewa halali

Haramu Uvuvi Mara.png Wavuvi 51 wasalimisha zana haramu Rorya, wapewa halali

Thu, 9 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wavuvi 51 waliokuwa wakitumia zana haramu kufanya shughuli zao ndani ya Mto Mara wamezisalimisha na kupewa zana halali za uvuvi.

Wavuvi hao wamesalimisha zana hizo baada ya elimu na kampeni liyoendeshwa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri) katika bonde la Mto Mara kwa lengo la kufanya ardhi oevu ya bonde hilo kuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kutokomeza uvuvi haramu ndani ya mto huo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zana halali na kuchoma zana haramu Jumatano Novemba 8, 2023 katika kijiji cha Kwibuse wilayani Rorya, Mkurugenzi wa Tafiiri kituo cha Mwanza, Dk Baraka Sekadende amesema kituo hicho kimetumia zaidi ya Sh14.6 milioni kununua zana hizo.

New Content Item (1)

“Tumeabaini uwepo wa uvuvi haramu katika mto huu ndio maana tukafanya kampeni pamoja na kuelimisha wavuvi juu ya mdhara ya uvuvi haramu lakini wengi bado hawajasalimisha zana zao pengine walidhani wangekamatwa lakini huu ni mwanzo mzuri,”amesema Dk Sekadende

Amesema ardhi oevu ya bonde hilo lenye ukubwa wa kilomita 387 za mraba ni miongoni mwa ardhi oevu kubwa kusini mwa jangwa la Sahara lakini inakabiliwa na changamoto mbambali ikiwemo shughuli za binadamu hivyo jitihada za makusudi zinahitajika kuifanya kuendela kuwepo vizazi na vizazi.

Ofisa Uvuvi Wilaya ya Rorya, Godfrey Bwathondi amesema mto huo kwa upande wa wilaya hiyo ina wavuvi 668 huku 340 wakitumia zana haramu za uvuvi.

Mratibu wa mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Mto Mara unaotekelezwa na Tafiri, Benedicto Kashindye amesema mradi huo unatarajia kupunguza vitendo vya uvuvi haramu katika mto huo kwa asilimi 60.

“Takriban watu 110,000 wanaoishi katika vijiji 27 ndani ya bonde hili wanategemea ardhi oevu kwaajili ya maisha yao lakini tayari tumeanza mikakati ikiwepo ya kuchukua zana haramu na kukabidhi zana halali na ili kufanikisha malengo haya mradi huu utakuwa shirikishi,”amesema

Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka ametoa muda wa siku 14 wote wanaojihusisha na uvuvi haramu kusalimisha zana zao kwa hiari.

“Rudisheni zana hizo ndani ya siku 14 hamtakamatwa, huu sio mtego… rudisheni kwa amani kabisa lakini wale wasiorudisha tafsiri yake wamedhamiria kuendelea na shughuli haramu na anayefanya shuguli haramu kuna namna ya kumrudisha kwenye mstari,”amesema

Chikoka amewataka wavuvi wilayani humo kujiunga kwenye vikundi ili kupewa mikopo inayotolewa na Serikali kwaajili ya kuboresha sekta yao.

“Pia nakuagiza ofisi uvuvi niandalie vikao nikutane na wavuvi wetu hawa ili niwafafanulie fursa za mikopo ya Serikali kuu ili waweze kujipanga na kuboresha shughuli zao kwa maslahi yao, jamii na taifa kwa ujumla,”amesema

Baadhi ya wavuvi wamesema ili kuondokana na zana za uvuvi haramu ipo haja ya Serikali kuzuia uingizwaji wa zana hizo kwenye soko.

“Hizi zana zinauzwa hadi hapa kijijini na kwa bei nafuu sasa ni vema Serikali kuanzia ngazi za vijiji hadi wilayani kushirikiana kutokomeza biashara hiyo ili zana hizo zisipatikane kabisa,”amesema Michael Tano

Chanzo: www.tanzaniaweb.live