Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wavulana Shule ya Palaka waomba choo kama wasichana

56304 Choopic

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kisarawe. Wanafunzi wa kiume wa shule ya msingi Palaka wilayani Kisarawe wameomba kujengewa choo ili waepuke kujisaidia vichakani baada ya matundu manne yaliyopo kutotosheleza mahitaji.

Wanafunzi hao walipaza sauti zao wakati Shirika la Plan International lilipokuwa likikabidhi mradi wa choo cha wasichana kilichogharimu zaidi ya Sh50 milioni.

Wakizungumza na Mwananchi Digital, leo, Jumatano, Mei 8, 2019, baadhi ya wanafunzi hao wamesema kama ilivyokuwa kwa wasichana nao hulazimika kujisaidia vichakani hasa wakati wa mapumziko kutokana na uchache wa matundu ya vyoo yaliyopo.

"Saa nne unaweza kupanga foleni hadi muda unaisha bado hujaingia chooni, inabidi ukajisaidie kule kwenye manyasi au kwa majirani, ila huwa wanatukataza, na sisi tunaomba kujengewa choo," amesema mwanafunzi wa darasa la sita, Adam Abdalah.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Innocent Muyebe amekiri uhaba wa matundu ya vyoo vya watoto wa kiume baada ya wa kike kujengewa vya kisasa.

"Ni kweli hawa wa kiume wanajisikia wanyonge kwa sababu wenzao wamejengewa, katika matundu manne yaliyopo kila tundu linatumika na wanafunzi 35, idadi kubwa lakini pia vyoo vimechakaa," amesema.

Mkurugenzi wa Plan International Kanda ya Kusini mwa Afrika, Charles Businge amesema mahitaji ya haraka ilikuwa ni kwa wasichana kulingana na maumbile yao kibaiolojia.

"Wavulana pia wanahitaji vyoo na tumeona jamii imeshaanza kuandaa matofali, hili tutashirikiana. Natamani nikija awamu nyingine mazingira haya yasiwe hivi," amesema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kisarawe, Musa Gama amesema kati ya mambo yaliyopewa uzito kupitia kampeni ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Joket Mwegelo ya tokomeza ziro ni ujenzi wa miundombinu ikiwamo vyoo.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz