Kibiti. Wavuvi wa mwamba wa Karumbi katika bahari ya Hindi uliopo kijiji cha Pombwe wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani nchini Tanzania wamevua samaki aina ya pweza tani moja ndani ya siku tatu.
Awali katika siku hizo tatu walikuwa wakivua kilo 27.
Pia, wamevua samaki aina kamba kochi (lobster) kilo 100.5 baada ya kufungua mwamba darasa wa Karumbi uliofungwa kwa muda wa miezi mitano ili kuwaacha samaki hao wakuwe lakini pia kuhifadhi rasilimali za bahari na kuepuka kuvua samaki wachanga.
Mafanikio hayo yametokana na ushirikiano miongoni mwa wasimamizi wa rasilimali za bahari na Pwani (BMU) wakishirikiana na halmashauri kwa kuwezeshwa na shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) wenye lengo la kuwasaidia wanajamii waweze kusimamia rasilimali zao wenyewe kwa kujipatia kipato pasipo kuharibu mazingira.
Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 3, 2019 mtendaji wa kata ya Kihongoroni, Rashid Sopo amesema kutokana na samaki hao kuwa na soko na umuhimu wake ilikuwa lazima kupatiwa hifadhi na kuwa wakubwa ili kuwapatia wavuvi na wanajamii (BMU) kipato kinachoridhisha lakini pia kijiji na halmashauri zinapata mapato.
Pia Soma
- Majaliwa amjibu kwa vitendo Mizengo Pinda
- Waliofukiwa na kifusi wafikisha siku ya tatu ardhini, Waziri Biteko awatuliza wananchi
- Waziri Lukuvi apongezwa kuwa mwanafunzi bora
Mvuvi Hassan Kijiko ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huo ambaye ameweza kuingiza zaidi ya Sh400,000 kwa siku moja kutoka Sh12,000 baada ya kuvua samaki aina ya kamba kochi ambao kilo mmoja mvuvi anapata Sh50,000 kutokana .
“Kutokana na uwekezaji wa miamba Karumbi imeleta faraja sana kwa wavuvi na wakazi wa kijiji cha Pombwe kwa sababu baada ya kuufungua baada ya miezi mitano tumepata kipato kikubwa ambacho ni kipato unakitafuta kwa muda wa mwezi mmoja kabla ya kufungwa mwamba,”anasema Kijiko
Fisa uvuvi shirikishi anayesimamia miradi ya WWF Kibiti na Manispaa ya Kigamboni,Jumanne Mohamed kutoka WWF amesema rasilimali za bahari zinapolindwa na kila moja zinasaidia kuhifadhi mazingira ya bahari kwa maendeleo endelevu ya mtu mmoja mmoja na Taifa na kuanzishwa kwa vikundi vya wasimamizi wa rasilimali hizo (BMU) zinazoundwa na wanavijiji wenyewe kumekuwa na mafanikio.
“Kwa sasa BMU ziko katika wilaya tano tunazofanya kazi, Manispaa ya Mtwara,Kigamboni, Mafia, Kibiti na Kilwa na wavuvi wenyewe wanaanza kuona faida za mradi lakini pia na usimamizi wa rasilimali kwa sababu wao ndio unawasaidia sana,”amesema Jumanne
Saumu Juma anasema, “Tunapokuwa tumefunga miamba kwa muda wa miezi kadhaa tunakuwa tunajihusisha na shughuli nyingine za kiujasiriamali kama ushonaji.”