Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wauawa na fisi wakisaka maji

Fisi.webp Wauawa na fisi wakisaka maji

Mon, 8 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WANAWAKE wanaoishi Kata ya Ngongwa wilayani Kahama, wamedaiwa kuwa hatarini kutokana na kuwapo na tishio la fisi pindi wanapofuata maji nyakati za usiku.

Imeelezwa kuwa tayari wanyama hao wameshasababisha vifo kwa wanawake wawili katika eneo hilo.

Diwani wa Ngogwa, Kamuli Mayunga, aliyasema hayo juzi wakati wa ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Kahama, iliyokuwa na lengo la kukagua mradi wa majisafi na salama ulioko katika kata hiyo.

Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka za Maji za Shuwasa, Kuwasa na Ruwasa, una thamani ya Sh. bilioni 2.4.

Mayunga alisema wanawake wa Ngongwa maisha yao yamekuwa hatarini kwa miaka mingi kutokana na uwapo na adha ya maji na hulazimika kuamuka majira ya usiku ili kufuata maji umbali mrefu, ambako njiani hukutana na fisi na kuanza kuwakimbiza.

Alisema wanyama hao wamekuwa wakiwajeruhiwa wananchi huku wawili wakiuawa.

“Maeneo yetu haya ya Ngongwa kuna fisi wengi sana kwa sababu ya uwapo na milima, na wamekuwa tishio kwa wanawake, wahatarisha maisha yao wanapokuwa wakifuata maji nyakati za usiku.

"Miaka miwili iliyopita, tulipoteza wanawake wawili sababu ya kushambuliwa na fisi hawa,” Mayunga alisema.

Baadhi ya wanawake wa Ngongwa akiwamo Celina Paulo, walikiri fisi hao kuwa tishio kwa maisha yao, huku wakiomba mradi huo wa maji ukamilike kwa wakati ili kuwaondolea adha hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (Shuwasa), Flaviana Kifizi, alisema mradi huo wa maji umekamilika kwa asilimia 95 na utaisha Agosti mwaka huu ukigharimu Sh. bilioni 2.4 na utanufaisha zaidi ya wakazi 1,000.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, alipongeza utekelezwaji wa mradi huo wa majisafi na salama, huku akiwataka wananchi waitunze miondombinu yake ili idumu kwa muda mrefu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live