Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watunishiana misuli stendi

32685 Pic+misuli Tanzania Web Photo

Fri, 21 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Hamsini ameapa kumsimamisha kazi ofisa mipango miji, Jonas Masangila kwa tuhuma za kubadili mipaka ya eneo la stendi.

Hata hivyo, Masangila amejibu tuhuma hizo akisema hayo ni majungu hayamtishi.

Mbele ya viongozi wa chama na Serikali wakiongozwa na mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu wakati wa ukaguzi wa mradi wa stendi ya wilaya, Hamsini alisema analazimika kuchukua hatua kali kwa ofisa huyo kutokana na kuhujumu mradi huo.

“Eneo hili limepimwa na halmashauri imelipia hati ingawa haijaja, tulipoanza ujenzi tumebaini eneo limevamiwa, vigingi vimebadilishwa na kuingizwa ndani, makanisa yakaingizwa ndani, hii kwa kweli ni hujuma dhidi ya maendeleo ya wilaya,” alisema.

Hamsini alisema halmashauri itawaondoa wote waliovamia eneo hilo. “Madiwani naomba tushikamane kwa hili mkiniacha niko tayari kubaki mwenyewe, siwezi kufanya kazi na mtu kama huyu lazima nimsimamishe kazi,” alisisitiza.

Alipoulizwa kwa njia ya simu, Masangila alisema hayo ni majungu. “Akuonyeshe ramani ya eneo kama anayo ili ujue ukubwa wake, awali ilikuwa wapi na imehamishwa hadi wapi.”

“Kama nimehamisha mipaka hiyo amechukua hatua gani, ana vielelezo gani, mimi niko hapa mbona hajaniambia, nasema andika kama alivyosema yeye lakini ni majungu tu,” alisema.

Naye Babu alisema aliyehujumu mradi huo lazima achukuliwe hatua kali kwa kuwa mradi huo una maslahi makubwa ya wilaya na unalenga kusukuma maendeleo ya wananchi.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Juma Porini alisema stendi hiyo itakuwa na vibanda 450 vya biashara na mpaka sasa wafanyabiashara 200 wameshaomba nafasi ya kufanya shughuli zao.



Chanzo: mwananchi.co.tz