Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishji 18 watimuliwa kazi

31125 Watumishipic TanzaniaWeb

Wed, 12 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Watumishi 18 wa Hifadhi ya Taifa ya kisiwa cha Rubondo mkoani Geita wamefukuzwa kazi kwa tuhuma za kujihusisha na uvuvi haramu.

Watumishi hao ambao ni askari 12 wa wanyamapori na mhifadhi mmoja wamefukuzwa kazi Septemba, 2018.

Wakizungumza jana Jumatatu Desemba 10, 2018 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu aliyetembelea hifadhi hiyo kwa ajili ya kujitambulisha, baadhi ya askari wamedai kutokuwa na uhusiano mzuri na uongozi wa hifadhi, kunasababisha watumishi kubambikiwa kesi.

Tumaini Kagine, askari wa wanyamapori amedai licha ya watumishi hao 18 kufukuzwa kazi bado askari wengine 14 hawajui hatima yao baada ya kuhojiwa kwa tuhuma za uvuvi haramu.

Amedai watumishi hao wamefukuzwa kazi baada ya taarifa ya vitendo vya rushwa dhidi ya viongozi hao kuripotiwa Takukuru huku watumishi hao wakituhumiwa kupeleka taarifa hizo.

Watumishi hao wameiomba wizara hiyo kuingilia kati, kuchunguza ili haki itendeke kwa madai kuwa hawana imani na uongozi, kudai kuwa waliowataja kuhusika na uvuvi haramu ni waendesha bodaboda.

Kwa upande wake Kanyasu amewataka kuzitambua sheria za hifadhi na kusimamia, kwamba sheria hizo hazitamuonea wala kumpendelea mtumishi yeyote.

Amesema madai ya watumishi hao yatafanyiwa kazi na kukitaka kikosi cha uchunguzi kuhusu ujangili kujiridhisha ili mtumishi anapohusishwa iwe isiwe uonevu.

Mhifadhi Mkuu wa kisiwa cha Rubondo,  Ignas Gala amesema sheria za uhifadhi ni kali na mtumishi akituhumiwa anachunguzwa na polisi, Takukuru na vyombo vingine vya usalama na ikithibitika anafukuzwa kazi.

Amesema katika uchunguzi wa awali watumishi 18 wamefukuzwa kazi na  wengine 14 wanachunguzwa na ikithibitika sheria itachukua mkondo wake.

Amesema sifa ya mtumishi wa umma ni kuwa mwadilifu na mwaminifu na kuwataka watumishi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za kazi na hakuna atakayeonewa.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz