Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishi watatu bodi ya maji wafukuzwa kazi

Mon, 23 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Watumishi watatu wa Bodi ya maji wilaya ya Igunga (Iguwasa) mkoani Tabora, wamefukuzwa kazi kwa tuhuma ya kula fedha za wateja wanazolipia ankara za maji.

Waliofukuzwa kazi mwishoni mwa wiki ni Justus Nshekanabo ambaye alikuwa kitengo cha usomaji mita za maji, Johnson Lugemalila aliyekuwa kitengo cha Uhasibu katika idara ya maji na Verdiana Nyamkara aliyekuwa kitengo cha uandaaji wa ankara za maji kwa wateja.

Wakizungumzia hatua ya kuwafukuza kazi watumishi hao, wajumbe wa bodi ya Iguwasa, Teddy Patrick na Hilda Kapaya, walisema wamefikia uamuzi huo baada ya kubaini watumishi hao walishindwa kuwa waaminifu kwa fedha wanazokusanya kwa wateja wanaotumia maji.

Walisema miongoni mwa tuhuma walizotuhumiwa watumishi hao ni pamoja na fedha Sh750,000 walizochukua kwa mfanyabiashara wa nyumba za kulala wageni, Msafiri Ndamo, ambapo fedha hizo hawakumpatia risiti na fedha hizo hazikufikishwa ofisini na badala yake walizitumia kwa maslahi yao binafsi.

Walisema pamoja na mteja huyo kulipa ankara za maji, lakini cha kusikitisha waliendelea kumdai malipo ikiwa ni pamoja na kumtishia kumkatia huduma ya maji kwenye nyumba zake na kuongeza kuwa wao kama viongozi hawako tayari kufanya kazi na watumishi wasio waaminifu.

Mmoja wa watumishi hao waliofukuzwa kazi, Johnson Rugemalila, alikiri kufukuzwa kazi na kusema yeye binafsi hajatafuna fedha yoyote ya wateja na kwamba anamwachia Mungu.

Meneja wa mamlaka ya maji safi na taka, mjini Igunga (Iguwasa), Raphael Melumba, alisema wateja wengi wameliwa fedha zao na watumishi hao akiahidi kutoa takwimu kamili kwenye kikao kijacho cha bodi ya maji.

Hivi  karibuni akiwa katika zira ya kikazi mkoani Tabora, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso alizitaka Mamlaka za Maji kutowabambikizia wateja wao ankara za maji huku pia akizitaka kutoa mafunzo kwa watumishi wake hasa wasoma mita ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Chanzo: mwananchi.co.tz