Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Adam Malima amemuagiza Katibu Tawala Mkoa huo kuwasimamisha kazi kwa siku saba akiwemo Mkuu wa Idara ya Ardhi Jiji la Mwanza Robert Phales, Ayubu Kasuka, Halima Nassor na Yuster Zephrine kuanzia leo Januari 13, 2023 ili kupisha uchunguzi kutokana na kuhusika na uuzaji wa ardhi bila kufata utaratibu.
Malima amesema kuwa Ofisi yake imeandika Barua kwenda TAMISEMl ya kuomba achukuliwe hatua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Sekiete Yahya kwa kukiuka Maelekezo ya kamati ya usalama ya Wilaya hiyo ya tarehe 28, 09, 2022 yaliyozuia uuzwaji wa viwanja namba 194 na 195 vilivyopo kwenye mtaa wa Rwegasore na wao kuamua kuviuza kwa Milioni 500 kila kimoja.
"Tumemkuta Mkurugenzi wa Jiji na Makosa makubwa sana ya kukiuka maelekezo ya Kamati ya Usalama Wilaya na ameonesha aheshimu kabisa Mamlaka zilizo juu yake kwa utovu huo wa nidhamu alioufanya ambapo alitengeneza hoja ya kuuza viwanja hivyo isivyo halali na tumebaini kuwa endapo vingeuzwa kwa njia ya Mnada basi vingeuzwa kwa milioni 800 kila kimoja."
Katika hatua ingine, Malima amesema Ofisi yake imeunda Kamati ya kuchunguza Sakata hilo kwa siku Saba itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Maadili wa Kanda ya ziwa Ndugu Godson Kweka huku ikihusisha wataalamu kutoka Ofisi za TAKUKURU, Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa pamoja na Ofisi ya Mashtaka (DPP).