Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuwachukulia hatua za kinidhamu Watumishi saba wa halmashauri ya wilaya ya Liwale mkoani Lindi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, na hivyo kuzorotesha utendaji kazi wa shughuli mbalimbali za halmashauri hiyo.
Waziri Mchengewa ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan alipotembelea wilaya ya Liwale kwa lengo la kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pia ameelekeza Maafisa wote wenye kesi za rushwa na ubadhirifu wasihamishwe vituo vyao vya kazi mpaka mashauri yao yanapokamilika.
"Afisa yeyote mwenye kesi ya uhujumu uchumi au ubadhirifu wakati kesi yake ikiendelea ataendelea kuchunguzwa mwenendo wake na hukumu yake ikitoka hatopewa tena jukumu la Ukuu wa Idara au Kitengo hadi mwenendo wake utakaporidhisha". amesema Waziri Mchengerwa
Watumishi waliotajwa kuchukuliwa hatua hizo za kinidhamu ni Sisty Njau ambaye ni Kaimu Mhandisi wa wilaya, Damasi Mumwi - mkuu wa Idara ya Maliasili, Mustafa Magembe - Mkuu wa Idara ya Kilimo na Ushirika, Vinsent Moyo - Mkuu wa Idara ya Ugavi na Ununuzi, Mohamedi Songolo - Mkuu wa Idara ya TEHAMA, Sadick Bakari Khatibu - Katibu wa Afya na Tunu Mtamaha - Afisa Ugavi na Ununuzi aliyehamishiwa halmashauri ya wilaya Kilwa.