Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishi darasa la saba wadai kutolipwa mishahara

54d6064eb08fa772c53acb1dd9bfa08c Watumishi darasa la saba wadai kutolipwa mishahara

Wed, 20 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATUMISHI wenye elimu ya darasa la saba walioondolewa kazini mwaka 2017 kwa kukosa cheti cha ufaulu kidato cha nne na baadaye kurejeshwa kazini Aprili 2018, bado hawajalipwa fedha za mishahara kwa kipindi walichoondolewa kazini.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), Rashid Mtima, aliyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano ya Kimataifa wa chama hicho, Shan Kibwasali, kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu , Jenista Mhagama.

"Mheshimiwa mgeni rasmi wanachama wetu wana changamoto nyingi za kiutumishi ambazo hazipo chini ya Wizara yako, lakini tunaomba utufikishie serikalini na tunaamini zitapatiwa ufumbuzi wa haraka"alisema Kibwasali.

Alisema, moja ya matatizo waliyonayo ni watumishi hao wa darasa la saba kutolipwa mishahara hiyo kwa kipindi ambacho waliondolewa kazini hivyo wanaiomba serikali imalize jambo hilo ili wanachama hao wa TALGWU wapate haki yao kwa mujibu wa sheria.

Kibwasali aliitaja kero nyingine kuwa ni wanachama wanaolipwa kwa mapato ya ndani kutolipwa mishahara kwa wakati na pia makato yao yanayohusiana na mishahara kutopelekwa katika taasisi zinazohusika.

"Kitendo hicho kinasababisha watumishi hawa kutokopesheka, kukosa huduma ya matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na kutopata mafao kipindi wanapostaafu,"alisema.

Kibwasali pia alisema kero nyingine ni baadhi ya maofisa utumishi kuwatoa wanachama wao kwenye makato ya ada ya uanachama na kuhamishia makato kwenye vyama vingine bila ridhaa na pasipo kuzingatia sheria.

"Kitendo hiki kinasababisha mtumishi kukosa huduma za msingi kutoka TALGWU, huleta mgogoro mahala pa kazi kati ya watumishi na viongozi wa vyama vya wafanyakazi katika ngazi ya matawi na hupunguza nguvu ya chama,"alisema.

Aidha, Kibwasali alisema kero nyingine ni ukiukwaji wa sheria unaodaiwa kufanywa na baadhi ya waajiri kwa kutoa maelekezo ya barua ya chama kipi wafanyakazi wanatakiwa kujiunga.

Alisema, kitendo hicho ni kunyume cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 06, ya Mwaka 2004.

Kibwasali alisema wanaiomba serikali iwaelekeze wakurugenzi wa Halmashauri ili kada ya maofisa watendaji wanaohusika na ukusanyaji wa mapato wapate mafunzo ya namna ya kutumia mashine za kukusanyia mapato (POS).

"Hali hii itasaidia na kuondoa kabisa suala la wanachama wetu wengi kufikishwa mahakamani kwa makosa ya upotevu wa fedha kutokana na kutojua matumizi sahihi ya mashine hizo"alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz