Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishi TFS wafundwa kuukabili uhalifu baharini

83617 PIC+MIKOKO Watumishi TFS wafundwa kuukabili uhalifu baharini

Thu, 14 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kamishna  wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Profesa Dos Santos Silayo amesema kuwa wakala huo umejipanga vema kukabiliana na uhalifu na ujangili ikiwemo utoroshaji wa rasilimali za misitu kwa njia ya bahari na nchi kavu.

Profesa Silayo ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya mbinu za kujiokoa baharini yaliyofanyika katika Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam (DMI) ambapo watumishi 15 wa TFS Kanda ya Kusini wanaofanya kazi kwenye misitu ya mikoko walihitimu.

"Niwapongeze watumishi ambao wamehitimu mafunzo haya muhimu, hii inamaanisha kwamba kwa sasa tunao askari na wakati huo huo ni mabaharia ambao wanakwenda kusimama kidete kwa kushirikiana na watumishi wengine kukabiliana na kila aina ya uhalifu hasa baharini.

 "Mafunzo haya yanatoa ujumbe kwa wahalifu kuwa sasa hawana nafasi. Tumejipanga na tutaendelea kujipanga siku hadi siku kwa kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wetu ikiwa ni pamoja na kuwafundisha mbinu za kisasa za kukabiliana na uhalifu,"amesema Profesa Silayo.

Amesema suala la usalama ni muhimu kwa watumishi wakati wa kutekeleza majukumu yao, hivyo mafunzo hayo ya mbinu za kujiokoa yatasaidia wanapokuwa katika mapambano kuwa na uhakika wa usalama wao.

Profesa Silayo amesema wakati watumishi hao wakipata mafunzo kuna changamoto zimeibuliwa ikiwemo ya uhaba wa vifaa, hivyo watahakikisha wanapata vifaa ili kuimarisha utendaji kazi wao na kufikia malengo huku akiongeza kuwa tayari kuna boti zimenunuliwa kuimarisha doria.

Msaidizi Misitu daraja la II, Herieth Balua amesema kuwa mafunzo hayo kwa vitendo yalishirikisha kwenda kujionea vifaa vya uokozi na namna vinavyotumika iwapo hatari itatokea. 

"Mafunzo haya ya mbinu binafsi za kujiokoa unapokuwa unafanyaka kazi katika maeneo ya bahari ikiwemo misitu ya mikoko ni kitendo au uwezo ama jitihada za mtu au kundi la watu zinazotumika kuokoa maisha iwapo janga lolote litatokea. Mafunzo haya ni muhimu kwa watendaji tunaofanya kazi katika maeneo ya misitu inayoota sehemu zenye maji.

Chanzo: mwananchi.co.tz