Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishi Halmashauri ya Geita wabanwa

3c1e829387807e7b28c782fabf95ab79.jpeg Watumishi Halmashauri ya Geita wabanwa

Mon, 20 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, ametoa wiki mbili kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuhamishia makazi yao karibu na ofisi za halmashauri hiyo.

Alitoa maagizo hayo hivi karibuni katika ziara yake ya kikazi katika Kijiji cha Kakubilo mkoani Geita ya kukagua maendeleo ya miradi ya Mpango wa Kunusur Kaya Maskini (TASAF). Mchengerwa alisema ana taarifa kuwa watumishi wengi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wanaishi Geita mjini umbali wa kilometa 53 kufika Kijiji cha Nzera zilipo ofisi za halmashauri hiyo.

“Bahati nzuri nina vyanzo vingi vya taarifa, ndani ya wiki mbili, watumishi wawe wamerudi huku, wafanye kazi na kuishi huku na wananchi. Kwa mtumishi ambaye hawezi kuishi na wananchi huku, nipewe taarifa zake ili tumtafutie kazi nyingine ya kufanya,”alisema Mchengerwa.

Aliongeza “Kama ambavyo Waziri Mkuu alitoa maelekezo, na mimi nasisitiza hapo hapo kwamba turudi tufanye kazi na wananchi, tuishi nao huku vijijini ili tupate tija ya kile kilichokusudiwa.” Pia aliwataka watumishi wa TASAF kushirikiana na Ofisi za Wakurugenzi katika kufanya mapitio na kuratibu upya wananchi wenye sifa ili waingizwe kwenye mfuko wa kujikwamua kimaisha.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo, alisema mpaka sasa halmashauri hiyo ina wanufaika wa TASAF takribani 7,000 na tangu kuanzishwa kwa mfuko huo, wilaya yake imeshapokea zaidi ya Sh bilioni 10.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live