Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishi 16 Moro ‘watema’ vizimba

A49a93269b43aad7d4f7f21fcf87e816 Watumishi 16 Moro ‘watema’ vizimba

Mon, 15 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATUMISHI 16 wa Halmashauri ya Manispaa Morogoro waliokuwa wakimiliki vizimba Soko Kuu la Chifu Kingalu, wamevirejesha na fedha walizochukua kwa wafanyabiashara waliowakodisha.

Watumishi hao walichukua vizimba hivyo na kuwatoza wafanyabishara Sh 50,000 kwa mwezi, badala ya kiwango cha Manispaa cha sh 20,000 kwa mwezi.

Serikali imetumia Sh bilioni 17.656 kujenga soko hilo lenye vizimba 900, maduka ya kawaida 304, maegesho, maduka makubwa na sehemu za mama lishe.

Ujenzi wa soko hilo ulianza Juni 20, 2018, baada ya kuvunjwa soko la zamani lililojengwa 1953.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, watendaji wa manispaa wakiongozwa na Meya na Mkurugenzi, kuanzia juzi walianza kutekeleza maagizo ya Rais John Magufuli kwa kuhakiki vizimba vyote.

Katika uhakiki huo, ilibainika kuwa watumishi 16 wa manispaa hiyo, walijimilikisha vizimba na kuvipangisha kwa wafanyanishara kwa bei ya juu.

"Kwa kifupi kuna maagizo matatu ya haraka katika soko hili, agizo la kwanza ni wafanyakazi wote wa serikali kuanzia wa mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na manispaa ambao wapo hapa kwenye vizimba na vioski waachie maeneo hayo, wawaachie wafanyabiashara wa kawaida" alisema Msulwa.

Agizo la pili linahusu baadhi ya wafanyakazi wa manispaa, waliochukua maeneo ya biashara na kuyapangisha wakati serikali inatoza wafanyabiashara wadogo Sh 20,000 kwa mwezi, lakini wao wanaongeza fedha na kuiibia serikali.

"Mnakumbua Rais alitaja jina la mmoja wa mfanyakazi wa Manispaa anaitwa Aika na agizo ni kwamba fedha hizo azitapike na hatua ya pili ni kuhakikisha kwamba wote waliohusika na vitendo hivyo nao wafanye hivyo hivyo kwa kipindi maalumu cha siku mbili "alisema Msulwa.

Agizo la tatu lilikuwa ni kuhakikisha soko linakuwa na utulivu na wafanyabiashara wanafanya kazi kwa utulivu na kero zimalizwe.

Alisema, katika uhakiki wamebaini baadhi ya viongozi wa zamani wa soko, walichukua vizimba vingi na wameambiwa wavirejeshe na tayari wameviachia.

Msulwa alisema tangu Rais Magufuli alipoondoka, walihakikisha aliyepewa agizo la ‘kutapika fedha’ anafanya hivyo na kukiri kwa maandishi.

Kwa mujibu wa Msulwa, walikaa na watumishi wa manispaa hiyo na kuwaeleza wachague kuendelea na ajira au kufuatilia masuala ya vizimba.

"Napenda kuwaambieni katika kipindi cha saa tatu tumepata orodha ya wafanyakazi wa mansipaa 16 ambao wenyewe wameandika majina yao na kusema wazi kabisa kuwa sisi tulikuwa na vizimba, hivi na sasa tunavitoa. Wapo wengine wachache walipata kuwa na vioksi na wengine maeneo mengine ya kibiashara lakini kwa ujumla wao wapo 16" alisema Msulwa.

Alisema, vizimba hivyo 16 wanavigawa kwa wafanyabiashara na wanafuatilia kuona kama watumishi hao, kama nyuma yake kulikuwa na biashara iliendelea.

“Tunafuatilia na ninawathibitishia kuwa kama itagungulika walipangisha basi watalazimika kutoa hizo fedha haraka iwezekanavyo, vinginevyo watakumbana na mkono wa sheria”alisema.

Alisema wamebadilisha uongozi wa soko hilo, kwa kuwa kulikuwa na makundi mengi, hivyo kusababisha matatizo makubwa.

Msulwa alisema bado kuna vioski 70 havina watu, hivyo aliwaomba wananchi na wafanyabiashara kuisaidia serikali kuona kama kuna mianya ya rushwa kwenye mchakato huo wa vioski. Alisema timu yake ipo kazini kuanzia asubuhi hadi usiku.

Mwenyekiti wa Soko la Chifu Kingalu, Khalid Mkunyegele, alimshukuru Rais Magufuli kwa neema kubwa aliyowaachia Morogoro na pia kwa kufungua soko hilo na kuona hali halisi ya wafanyabiashara.

Alimshukuru Rais kwa kuwaondolea ushuru waliokuwa wakitozwa na manispaa wanapoingiza bidhaa ndani ya soko na kuanzia siku hiyo hawatozwi tena.

Mfanyabiashara, Said Alawi, ambaye alikuwa amekodishwa kizimba na mtumishi wa Manispaa aliyemtajwa kwa jina la Aika kwa Sh 50,000 na kukilipia kwa muda wa miezi mitatu, amerejeshewa fedha zake na kumilikishwa kizimba namba 154.

"Namshukuru Mheshimiwa Rais alipotembela Soko Kuu la Morogoro kusikiliza kero za wanyonge na nilipomfikishia kero yangu ya kukodishiwa kizimba kwa shilingi 150,000 kwa muda wa miezi mitatu mfanyakazi wa manispaa, aliagiza nirudishiwe fedha yangu na tayari nimerusishiwa na kumilikishwa kizimba, ninasubiri uhakiki tu ili nipatiwe mkataba wangu niweze kulipa Sh 20,000 kwa manispaa kila mwezi na ushuru wa kuingiza bidhaa ndani ya soko kuu umeondolewa. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais" alisema Alawi.

Februari 11 mwaka huu akiwa mkoani Morogoro kuzindua soko hilo, Rais Magufuli aliagiza wafanyakazi wa manispaa ya Morogoro na taasisi nyingine za serikali, wanaomiliki vizimba kwenye soko kuu hilo na kuwakodishia wafanyabiashara kwa Sh 50,000 kwa mwezi, ' wazitapike' haraka kama wanataka kuendelea kuwa watumishi wa umma.

Alitoa siku saba kwa Mkuu wa Mkoa, Loata Ole Sanare kushirikiana na mkuu wa wilaya, uongozi wa manispaa, meya na mbunge wa jimbo la Morogoro Mjini, kumaliza kero za wafanyabishara wa soko hilo jipya.

Chanzo: habarileo.co.tz