Wakazi wa Mtaa wa Mbutu Mkwajuni, Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam wamejikuta wakitumia Sh4,000 kufuata sokoni fungu la dagaa la Sh1,000 kutokana na ubovu wa barabara.
Mkazi wa eneo hilo, Frank Ngunda amesema hayo leo Januari 11, 2024 alipokuwa akitoa malalamiko yao kuhusu ubovu wa barabara katika eneo lao.
Ngunda amesema kutokana na ubovu huo wa barabara, gharama za maisha zimeongezeka huku akitolea mfano wanavyolazimika kukodi bodaboda kwa Sh3,000 kwa ajili ya kufuata dagaa wa Sh1,000, hivyo wanajikuta wakitumia Sh4,000.
“Tunaiomba Serikali katika hili, ituangalie kwa jicho la huruma kututengenezea barabara kwa kuwa tumekuwa tukiteseka kwa muda mrefu,” amesema Mbunda.
Ipuli Sagula, amesema ubovu huo wa barabara umechangiwa pia na malori ya kubeba mchanga yanayopita hapo, hali iliyosababisha waifunge ili yasipite.
Sagula ambaye pia ni mjumbe wa Serikali ya mtaa, amesema nyumbani kwake kuna kijana wake alivunjika miguu, lakini kila wakienda hospitali inabidi wambebe mgongoni ili kuzifikia bajaji zilipo, jambo ambalo ni mateso kwao.
Akieleza sababu ya kufunga barabara, Shamimu Shabani amesema kwa muda mrefu kero hiyo imekuwa haifanyiwi kazi kwa kuwa ukiacha bodaboda kupita kwa tabu lakini gari ndogo ndio hazipiti kabisa na kwamba hivi karibuni kuna mwanamke alijifungulia nyumbani kutokana na kukosa usafiri.
“Haya malori tunajua yanaiingizia Serikali hela yanapokuja kubeba mchanga hapa, hivyo wakiyaona hayafanyi kazi na kuwapelekea hela labda watatukumbuka,” amesema Shamimu.
Hata hivyo, Mwananchi iliwatafuta Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura) kujua mpango wao kuhusu barabara hiyo, Meneja Msaidizi, Edger Kimaro, alikiri kuifahamu changamoto hiyo na kueleza kuwa tayari wameanza kuishughulikia.
“Ni kweli kuna hiyo changamoto na kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Kigamboni, watu wa mazingira na Jeshi la Polisi tulifika kujionea hali halisi ni kweli kunahitajika matengenezo.
“Hata hivyo, awali kuna taarifa ambazo wananchi walikuwa hawajaziwasilisha kwetu, lakini kupitia Serikali ya mtaa wao tulizungumza pamoja na watu wa malori hivyo tukakubaliana na ngazi ya juu kuirekebisha hiyo barabara,tunawaomba tu wawe na subra,”amesema Kimaro.