Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu wenye albino walalamikia majina yanayowavunjia utu na thamani yao

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Baadhi ya makabila hapa nchini yamelalamikiwa kwa kutumia majina yanayodhalilisha utu na thamani ya watu wenye ualbino.

Wamesema hali hiyo inachangia kuongezeka kwa hali ya unyanyapaa na kuendelea kwa  matukio ya mauaji ama ukatili kwa watu hao.

Malalamiko hayo yametolewa leo Jumatano Mei 29, 2019 na mlagabishi kutoka shirika hilo, Kondo Sefu kwenye mafunzo ya siku mbili kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.

Sefu amesema wameona kuna haja ya kutoa elimu kwa wahariri wa vyombo vya habari ili wayafahamu matumizi sahihi lugha wakati wa kuchakata habari zinazowahusu watu wenye ualbino.

 

Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto za matumizi ya majina sahihi ya makundi ya watu wenye ulemavu na kutolea mfano majina wanayoitwa watu wenye albino kuwa ni pamoja na walemavu wa ngozi, zeruzeru na albino na hivyo majina hayo kudhalilisha utu na heshima yao.

Pia Soma

Hata hivyo, amelishukuru Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) kwa kutoa jina sahihi la ‘watu wenye ualbino’ hivyo alivitaka vyombo vya habari kutumia jina hilo katika habari mbalimbali zinazowahusu.

 

Awali, akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo la Under the Same Sun, Berthasia Ladislaus amesema shirika hilo kwa kushirikiana na Serikali, limesaidia kupunguza matukio ya mauaji na vitendo vingine vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino.

Amesema katika kipindi cha Januari hadi Mei, kumekuwa na matukio mawili tu ya matishio ya utekaji wa watu wenye ualbino katika maeneo ya Ngorongoro na Kwimba.

Amesema watu wasiojulikana walitaka kuwadhuru watoto wawili wenye ualbino, hata hivyo majaribio hayo hayakufanikiwa.

Aidha, Mkurugenzi huyo ameipongeza serikali kwa kuchua hatua za dharura ikiwemo ya kuwahamishia watoto wenye ualbino kwenye baadhi ya shule maalumu za Buhangija iliyopo mkoani Shinyanga na Mitindo iliyopo Mwanza kwa sababu za kiusalama.

Akizungumzia mafanikio ya shirika hilo tangu lilipoanzishwa mwaka 2009, Berthasia amesema wameweza kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wenye ualbino kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu.

Amesema kupitia ufadhili huo mpaka sasa, tayari wameshasomesha watoto zaidi ya 415 na wanafunzi 190 walishahitimu kwa ngazi mbalimbali na wengine wameshapata ajira katika maeneo tofauti.

Naye Ofisa sheria wa shirika hilo, Maduhu Wiliam amesema kutokana na elimu inayotolewa kwa watu wa kada tofauti, watu wenye ualbino wameweza kupata haki zao ambazo ni pamoja na haki ya kuoa ama kuolewa na mtu asiyekuwa na ualbino na pia haki ya kusoma na kupata ajira mahali popote.

Chanzo: mwananchi.co.tz