Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu wawili wafa kwa kufukiwa kifusi mgodini

10580 Pic+kifusi TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tarime. Watu wawili wamefariki kwa kufukiwa na kifusi wakati wakichimba dhahabu katika machimbo yaliyopo mtaa wa Buguti, kata ya Turwa mjini Tarime.

Kamanda wa polisi kanda maalumu Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5:00 asubuhi.

Aliwataja waliofariki kuwa ni Bisaku Chacha (19) na Charles Mairo (18).

Alisema waliingia kwenye shimo lililokuwa limeachwa siku nyingi wakitafuta dhahabu kisha wakafukiwa na kifusi.

Naye mzazi wa Charles, Mairo Wembe alisema hakuamini wakati alipopata taarifa hizo kwa kuwa alikuwa Nyamongo alikohamia kwa muda kwa ajili ya utafutaji.

Alisema aliamini baada ya kufika nyumbani.

“Nilimwachia nyumba nikaenda kutafuta riziki, alianza kununua mabati kwa ajili ya kuezeka nyumba kupitia biashara yake ya ndizi lakini baadaye alikwenda mgodini ambako ndiko mauti yamemfika,” alisema Wembe.

Ofisa madini mkoa wa Mara, Nyaisara Mgaya alisema ofisi yake haina taarifa ya uwapo wa mgodi huo kwa kuwa Tarime inayo migodi miwili ya Kogete na Mgabiri, hivyo kuahidi kufanya utaratibu wa kufika eneo hilo kujiridhisha na usalama wake.

Akizungumzia tukio hilo, mkazi wa mtaa wa Kibuye, Werema Marwa alisema vijana hao waliondoka wenyewe na kuingia shimoni bila kuwa na mtu mwingine nje ndiyo maana walipofukiwa walikosa msaada.

Alisema walishtukia tukio hilo saa 12:00 jioni baada ya kufika eneo hilo na kutambua viatu vyao na kuvichukua kuvipeleka nyumbani.

Chanzo: mwananchi.co.tz